Jumatatu , 4th Nov , 2019

Baada ya kukamilika kwa mchezo wa pili wa kuwania kufuzu Kombe la Shirikisho barani Afrika kati ya Pyramids FC na Yanga, kocha wa Pyramids ameipa sifa kubwa Yanga kutokana na uwezo waliouonesha.

Mchezo wa Pyramids FC na Yanga

Mchezo huo uliopigwa Jijini Cairo nchini Misri usiku wa Novemba 3, ulimalizika kwa wenyeji Pyramids kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 na kuisukuma nje Yanga kwa jumla ya mabao 5-1.

Akizungumza baada ya mchezo huo, kocha wa Pyramids, Sebastien Desabre amesema kuwa timu yake imekoshwa na kiwango cha Yanga katika mchezo huo, huku akiwasifia wachezaji wake waliopelekea ushindi katika mechi zote mbili.

"Baada ya mchezo, Yanga ambao ni moja ya mabingwa wa Tanzania wamecheza vizuri na pia wenyewe wamekubali juu ya uwezo wa timu yangu. Tulistahili kushinda mabao zaidi ya matatu kwenye mchezo huu", amesema Desabre.

"Abdullah Al Saeed na Eric Traore ni wachezaji wazuri sana ambao wanaweza kucheza sehemu yoyote", ameongeza.

Kwa matokeo hayo, sasa Yanga inatupwa nje ya michuano huku Pyramids FC ikifanikiwa kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kwa mara ya kwanza katika historia ya timu hiyo ambayo imefanya uwekezaji mkubwa katika miaka ya karibuni.