Alhamisi , 16th Jun , 2016

Jose Mourihno kocha mpya wa United anataraji kubisha hodi na kufanya usajili wa mchezaji raia wa Poland Robert Lewandowski ikiwa ni harakati za kukijenga upya kikosi chake na kurejesha heshima ya Old Trafford.

Mshambuliaji wa Bayern Munich na Poland Robert Lewandowski.

Mshambuliaji wa kati wa Poland Robert Lewandowski ambaye kwa sasa hana nafasi ya uhakika ndani ya Bayern Munich sasa anahusishwa na kuhamia katika ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu ujao.

Mshabuliaji huyo wa Bayern yuko kwenye kikosi cha nchi yake ambacho kitapambana na Ujerumani katika mchezo wa hii leo wa kundi C Mjini Paris.

Kila wakati amekuwa akihusihwa na kutua Manchester United, lakini aliendelea kutoa nafasi zaidi ya kubakia katika timu yake ya zamani ya Borussia Dortmund na miaka miwili iliyopita alifanya hivyo akiwa Munich.

Mchezaji huyo mwenye miaka 27 pamoja na kuwa hivi sasa yuko kwenye mazungumzo ya kuongeza mkataba na waajiri wake wa sasa Bayern lakini amewaambia marafiki zake wa karibu kuwa yuko tayari kusikiliza ofa kutoka timu nyingine.

Ndoto za Lewandowski ilikuwa ni siku moja kucheza Real Madrid na amekuwa akihusishwa pia kutaka kujiunga na timu hiyo inayotumia dimba la Bernabeu iwapo ikiwa tayari basi hatokataa.

Shabiki huyo wa Liverpool wakati akiwa mdogo amekiri kuwa anatamani kufanya kazi tena na kocha wake wa zamani wakati akiwa Dortmund Jurgen Klopp ambaye anainoa Liverpool kama timu hiyo itafanikiwa kucheza michuano ya Uefa Champion League.

Lewandowski ambaye ameifungia Bayern mabao 47 katika michezo 57 ya Bundesliga katika misimu yake miwili ndani ya timu hiyo maarufu kama Bavaria anaweza kusaini mkataba mpya kama hatopata ofa nzuri kutoka sehemu nyingine lakini inafahamika kuwa mchezaji huyo anataka kuondoka ili kwenda kupata changamoto mpya mahali pengine.

Na tayari kuna taarifa kuwa kocha mpya wa United Mreno Jose Mourinho yuko mbioni kupeleka maombi rasmi Munich ili kutaka kuwa wa kwanza kuona anafanikiwa kufanya usajili wa mshambuliaji huyo mwenye uwezo wa kupachika mabao.