Maazimio 4 ya TPBL, kufuatia michezo kusitishwa

Jumatano , 18th Mar , 2020

Bodi ya Ligi Tanzania (TPBL) imetangaza maazimio 4 baada ya Serikali kusimamisha shughuli za michezo nchini kwa kipindi cha siku 30 kutokana na mlipuko wa virusi vya Corona.

Mashabiki wa klabu ya Simba uwanjani

Katika kikao kilichofanyika leo, Bodi imeazimia mambo manne ili kuhakikisha baada ya muda uliowekwa na Serikali kupita, ligi inaendelea katika mazingira salama.

Ofisa Mtendaji wa Bodi (CEO), Almas Kasongo amesema TPBL imetangaza kuunga mkono uamuzi wa Serikali kusitisha shughuli zote za michezo kwa mwezi mmoja ili kudhibiti maambukizi ya visusi vya Corona na azimio la pili, wachezaji wote walamika kupimwa virusi vya Corona kabla ya kuendelea na mechi.

Azimio la tatu, michezo itachezwa bila ya mashabiki baada ya siku 30 za kusimamishwa kwa mashindano yote nchini katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa Corona ulioingia nchini.

Aidha, Bodi imeazimia kuwa ligi imalizike ndani ya mwezi Juni ili kutoa nafasi kwa timu zitakazoiwakilisha nchi kimataifa kuendelea na mchakato wa mashindano ya CAF lakini pia bodi itaendelea kusimamia afya kipindi hiki cha tahadhari ya Corona.