Alhamisi , 2nd Sep , 2021

Tukiendelea kuhesabu siku kuelekea Tamasha la Simba Day, Kaimu Ofisa Habari wa timu hiyo, Ezekiel Kamwaga ameweka wazi kuwa maandalizi yapo vizuri na watafanya kitu kikubwa.

Kaimu Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga.

Simba day ni siku maalumu ambayo hutumika kwa ajili ya kuwatambulisha wachezaji waliosajiliwa, benchi la ufundi na wale ambao walikuwa katika kikosi kwa msimu wa 2020/21.

Kwa kikosi cha Simba ni wachezaji wawili ambao watakosekana nao ni Luis Miquissone ambaye yupo zake Al Ahly na Clatous Chama ambaye yupo zake ndani ya RS Berkane.

Simba Day inatarajiwa kufanyika Septemba 19, Uwanja wa Mkapa ambapo pia uzi mpya wa Simba utaonyeshwa ukiwa umevaliwa kwa mara ya kwanza na unatarajiwa kuzinduliwa Jumamosi ya Septemba 4 mwaka huu.

Kamwaga amesema:"Maandalizi ya Simba Day yanakwenda vizuri na tupo tayari kwa ajili ya kuwaonesha mashabiki namna gani tunafanya mambo mazuri kwa ajili yao”.

“Simba Day ya mwaka huu itakuwa kubwa. Mpaka sasa tumeshapokea maombi ya timu ambazo zimeshashinda ubingwa wa Afrika zaidi ya mara mbili. Nawahakikishia Simba itacheza na timu kubwa sana barani Afrika katika Simba Day 2021.” 

Tayari wapinzani wao wa jadi Yanga wao siku yao ya Mwananchi Day iliweza kufanyika na utambulisho wa jezi pamoja na wachezaji uliweza kufanyika kilele chao ilikuwa ni Agosti 29,  2021 Uwanja wa Mkapa.