Jumanne , 28th Jun , 2016

Baada ya kuahirishwa kwa mara kadhaa michezo ya mashindano maalumu ya wanamichezo mabingwa wa michezo ya sanaa mbalimbali za mapigano nchini sasa ni rasmi michuano hiyo itafanyika kati ya Julai mwishoni ama Agosti mwanzoni mwaka huu Jijini Dsm.

Waziri mkuu wa zamani wa Tanzania Mizengo Pinda akiwakabidhi makombe washindi wa mchezo wa mapigano.

Akizungumza hii leo katibu mkuu wa chama cha mchezo wa Wushu Tanzania TWA Sempai Gola Kapipi amesema mashindano ya mabingwa wa mabingwa kwa michezo yote ya sanaa za mapigano yatafanyika mwishoni mwa mwezi Julai ama mwanzoni wa Agasti mwaka huu.

Kapipi ambaye pia ni kocha wa mchezo huo amesema michuano hiyo itashirikisha washiriki mabingwa wa michezo tofauti ya sanaa za mapigano kama Wushu yenyewe, Kung Fu, ngumi, Karate, Judo, Taekwando, ngumi na mateke, Shaoling, na aina nyingine nyingi za sanaa za mapigano.

Aidha Kapipi amesema lengo la kuanzisha shindano hilo ni kutaka kuonyesha utofauti na ufanano wa sanaa hizo katika uchezaji wake na sheria za kuongoza mchezo husika, pili ni ni kutaka kujenga umoja na ushirikiano baina ya wanamichezo wa sanaa hizo tofauti za mapigano na mwisho ni kukata mzizi wa fitna baina ya wachezaji wa michezo hiyo hapa nchini baada ya kila mmoja kutamba sanaa yake ndiyo bora zaidi hivyo kuwepo na shindano baina yao ndiyo itakuwa suluhusho la kutambua ni mchezo yupi zaidi ya mwingine.

Akimalizia Kapipi ametoa wito kwa wadau na makampuni mbalimbali kuhakikisha wanatumia fursa ya mashindano hayo kutangaza biashara zao kupitia udhamini wa mashindano hayo ikiwa ni pamoja na kusaidia kuinua michezo hiyo ya mapigano ambayo imekuwa ikifanya vema katika medani ya kimataifa ukilinganisha na michezo mingine ambayo imekuwa ikipata udhamini mkubwa lakini imekuwa ikifanya vibaya.