Jumatatu , 15th Oct , 2018

Kiungo Juma Mahadhi ataendelea kukosekana zaidi Yanga SC baada ya mwishoni mwa wiki hii kurejeshwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwaajili ya matibabu zaidi.

Juma Mahadhi akijaribu kumtoka mchezaji wa Township Rollers

Afisa Habari Msaidizi wa Yanga SC, Godlisten Anderson 'Chicharito' amesema kwamba Mahadhi alilazimika kurejeshwa Muhimbili kwa matibabu zaidi kufuatia kuumia goti, Agosti mwaka huu.

Baada ya matibabu hayo, Chicharito amesema kwamba Mahadhi amepewa wiki mbili za kuendelea kupumzika bila kufanya mazoezi kabla ya kurejea hospitali kufanyiwa uchunguzi mwingine.

Ikumbukwe kiungo huyo mshambuliaji, Juma Mahadhi aliumia Agosti 19 mwaka huu kwenye mchezo wa Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger ya Algeria Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Yanga SC ilishinda 2-1, mabao yake yakifungwa na Deus Kaseke dakika ya 43 na Mkongo Heritier Makambo dakika ya 47, kabla ya Abderrahmane Meziane kuwafungia USM Alger dakika ya 53.

Na Mahadhi aliingia kipindi cha pili akitokea benchi kwenda kuchukua nafasi ya kiungo Pius Buswita, lakini kwa bahati mbaya hakumaliza mchezo baada ya kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Ibrahim Ajib.