Alhamisi , 23rd Mei , 2019

Binti wa darasa la saba, shule ya msingi Kashenge katika Manispaa ya Bukoba, amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera akiuguza majeraha anayodai kuyapata baada ya kuunguzwa kwa maji ya moto na mama yake wa kambo.

Mwanafunzi aliyeunguzwa maji ya moto

Akizungumza kwa shida akiwa wodini, binti huyo mwenye umri wa miaka 16, amesema kuwa alimwagiwa maji ya moto na mama huyo kwa sababu alipika viazi bila kuambiwa.

Akizungumza na www.eatv.tv, Afisa Muuguzi Msaidizi wa wodi namba kumi upande wa upasuaji, Edith Ezekiel amesema kuwa walimpokea binti huyo jana akiwa ameunguzwa mkono wa kulia, titi na sehemu za bega,  na kuwa hali yake kwa sasa sio mbaya na anaendelea na matibabu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi amesema kuwa atatoa taarifa rasmi kesho kuzungumzia tukio hilo ambalo tayari limeripotiwa polisi na kufunguliwa jalada la kujeruhi namba RB/2466/19.