Jumatatu , 29th Jul , 2019

Uongozi wa klabu ya Simba umesema kuwa kuanzia tarehe 31 Julai 2019, itazindua mambo makubwa matatu kwa ajili ya klabu na mashabiki wake kuelekea wiki ya Simba Day itakayohitimishwa Agosti 6.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori

Kauli hiyo imezungumzwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Crescentius Magori katika mkutano na waandisi wa habari Jijini Dar es Salaam leo, ambapo amesema matukio hayo yatazinduliwa kuanzia kwenye ufunguzi wa wiki ya Simba Day, Julai 31 hadi kilele chake Agosti 6.

"Kwanza kabisa wiki ya Simba Day itazinduliwa tarehe 31 Julai, siku ambayo mabingwa wa nchi watarejea kutoka Afrika Kusini. Kitu cha pili ambacho kitafanyika ni kusaini mkataba wa jezi na vifaa vya mazoezi na kampuni ambayo tumeingia nayo mkataba wa miaka miwili", amesema Magori.

"Siku hiyohiyo tarehe 31 kuamkia Agosti 1 saa sita usiku, tunaomba Wanasimba wote wawe kwenye mtandao na kwenye mitandao ya kijamii ya Simba, tutazindua jezi mpya ya klabu kwa msimu wa 2019/20. Tutazindua jezi za ugenini, za nyumbani na ambazo hazina upande wowote", ameongeza Magori.

Pia amesema kuwa klabu hiyo itazindua mfumo mpya wa kadi za uanachama wa klabu hiyo pamoja na kadi za mashabiki ambazo zitakuwa katika mfumo wa kisasa uliounganishwa na benki. Pia itazindua wimbo maalum wa klabu kuelekea mchezo wa Simba Day dhidi ya Power Dynamos ya Zambia.