Jumatano , 8th Jul , 2020

Aliyewahi kuwa mchezaji mashughuli wa klabu ya Yanga,Sunday Manara,baba mzazi wa afisa habari wa klabu ya Simba Hajji Manara ametoa angalizo kwa uongozi wa klabu yake juu ya aina ya wachezaji wanaowasajili.

Nyota wa zamani wa klabu ya Yanga,Sunday Manara(pichani)katika mahojiano na EATV kuhusiana na mchezo baina ya Simba dhidi ya Yanga siku ya Jumapili uwanja wa Taifa.

Nyota wa zamani wa klabu ya Yanga,Sunday Manara amewataka viongozi wa klabu yake kutafuta njia nzuri ya kuwasajili wachezaji ambao watajitolea kuipigania timu kuliko kuweka maslahi yao binafsi.

Manara ambaye ndiye baba mzazi wa mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa Simba Hajji Manara,amesema hapendezwi na tabia za mchezaji Banard Morrison ambaye ameonekana akiiyumbisha klabu yao katika kipindi hiki muhimu wanachohitaji kuipata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa.

Amesema kwamba anasikitishwa na jinsi mchezaji huyo wa Ghana anavyoiendesha klabu,akiamini kwamba enzi zao hakuna mchezaji aliyekua juu ya klabu,pia akaenda mbali zaidi akisema kulikua na utaratibu mzuri wa kutengeneza wachezaji bora kwa manufaa ya timu kuliko sasa.

Mshambuliaji huyo aliyewahi kutikisa katika soka la kitaifa na kimataifa,amesema miaka ya hivi karibuni kumekosekana utaratibu wa kulea na kuvikuza vipaji vya hapa nchini,jambo linalopelekea watumie fedha nyingi kusajili wachezaji wa kigeni ambao hawana mapenzi ya dhati na klabu.

Ikumbukwe Benard Morrison ameripotiwa kutotambua mkataba wa miaka miwili unaotajwa ameusaini akishinikiza kuondoka katika klabu ya Yanga kwa kuwa amepata timu nyingine baada ya kudumu jangwani kwa miezi sita pekee.