Jumatatu , 8th Jan , 2018

Afisa Habari wa  Simba SC Haji Manara, ameeleza kupokea kwa masikitiko makubwa msiba wa mlinzi wa zamani wa timu ya Yanga na timu ya taifa Athumani Juma maarufu kama 'Chama'.

Athumani Juma ambaye alianzia maisha ya soka kwenye klabu ya Pamba FC ya Mwanza amefariki usiku wa kuamkia leo katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya ugonjwa wa Kiharusi.

''Simba imesikitishwa sana na taarifa za msiba wake na tunaungana na wenzetu wa Yanga kuhakikisha tunampuzisha vyema katika nyumba yake ya milele'', amesema Manara.

Manara amesema yeye binafsi alipata nafasi ya kumshuhudia marehemu Chama tangu akiwa Pamba FC akicheza kama mlinzi wa pembeni miaka ya 1979, kabla ya mwaka 1981 kutua Yanga na kuanza kucheza kama beki wa kati ambapo alicheza kwa mafanikio makubwa.

Moja ya matukio makubwa ambayo Haji mtoto wa mchezaji wa zamani wa Tanzania Sunday Manara, amesema anayakumbuka sana kutoka kwa marehemu Chama ni namna alivyomsubiri mshambuliaji wa Simba Zamoyoni Mogela ‘Golden Boy’ nje ya uwanja wakati akitibiwa ili arudi uwanjani kwenye moja ya michezo ya Simba na Yanga kwa wakti huo.

Chama ambaye ni mzaliwa wa Mwanza, katika enzi zake za uchezaji alifikia hatua ya kuwa nahodha wa Yanga na timu ya taifa, akicheza na katibu mkuu wa sasa wa klabu hiyo Charles Mkwasa. Nyota huyo alistaafu soka mwaka 1990.