Ijumaa , 21st Sep , 2018

Hali si shwari hivi sasa katika klabu ya Simba kufuatia kichapo cha 1-0 ilichokipata kutoka kwa Mbao Fc katika mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara, katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza hapo jana.

Mashabiki wa Simba wakiwa jukwaani.

Mashabiki walioshuhudia mchezo huo ndani na nje ya uwanja waliibua hisia zao dhidi ya kocha wa timu hiyo Mbelgiji, Patrick Aussems kuwa ndiyo sababu ya timu hiyo kutofanya vizuri katika ligi msimu huu kutokana na kiwango kibovu wanachokionesha uwanjani.

Shinikizo hilo limemlazimisha afisa habari wa klabu hiyo, Haji Manara kuwaomba mashabiki kupiti ukurasa wa Instagram huku akisisitiza kuwa klabu inajipanga kufanya maamuzi stahiki katika kipindi hiki ili kuweza kuinusuru klabu.

Katika tukio ambalo si la kiungwana na lisilo la kimichezo, walionekana baadhi ya mashabiki video fupi mbalimbali wakiwarushia makopo ya maji baadhi ya wachezaji, makocha na viongozi wa klabu hiyo akiwemo, Haji Manara mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo.

Mpaka sasa Simba imekwishapoteza alama nne katika mechi mbili mfululizo za ugenini, ikipoteza alama mbili kwa kutoka sare na Ndanda Fc katika mchezo wa wikiendi iliyopita katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.

Mashabiki wengi wa Simba wamekuwa hawaridhishwi na kiwango cha uchezaji cha kikosi cha Simba tangu kocha, Patrick Aussems alipojiunga na timu hiyo kabla ya msimu huu kuanza, wakitaka kocha msaidizi, Masoud Djuma kupewa nafasi hiyo kutokana na kufanikiwa kwa kipindi kifupi alipokuwa kocha mkuu wa timu ambapo timu ilionekana kucheza mpira wa kuvutia na kufunga magoli mengi.

Mchezo ujao, Simba itakuwa ugenini kucheza na Mwadui Fc ya Shinyanga, mchezo ambao utakuwa ni wa tatu mfululizo kwa klabu hiyo kucheza ugenini msimu huu.