Jumanne , 16th Oct , 2018

Kocha wa Manchester United Jose Mourinho huenda akaukosa mchezo wa EPL dhidi ya Chelsea, utakaopigwa Oktoba 20, 2018, baada ya kushtakiwa na FA kwa tuhuma za kutoa matusi.

Jose Mourinho akitembea baada ya mechi dhidi ya Newcastle United.

Mourinho alinaswa na kamera akitamka maneno ya matusi baada ya mchezo wa Manchester United dhidi ya Newcastle United Oktoba 6, mchezo uliomalizika kwa United kushinda mabao 3-2 ikitokea nyuma baada ya kufungwa mabao 2-0.

Kwa mujibu wa taarifa ya FA iliyotolewa leo imeeleza kuwa jalada la Mourinho limefikishwa kwenye kamati ya nidhamu na maadili ili kujadili matamshi yake ambayo hayajasikika kwa sauti lakini wataalam wa lugha za ishara wanaamini Mourinho alitukana.

Video mbalimbali zinamwonesha Mourinho akitembea huku akirusha mkono wa kulia na mdomo ukiwa na ishara ya kutoa maneno baada ya timu yake kufanikiwa kutoka kufungwa mabao 2-0 kipindi cha kwanza na kushinda 3-2 katika mchezo huo.

Mourinho amepewa muda hadi saa 12:00 jioni Oktoba 19 kuwasilisha utetezi wake. Endapo atapatikana na hatia anaweza kufungiwa kukaa kwenye benchi kwa mechi kadhaa na anaweza kuaanza na mechi dhidi ya Chelsea.