Mbrazil ashangazwa na mashabiki wa Simba

Jumatano , 7th Aug , 2019

Kiungo mpya wa klabu ya Simba, Gerson Fraga Vieira ameelezea jinsi alivyoshangazwa na mashabiki wa klabu hiyo waliojitokeza katika mchezo wa Simba Day hapo jana.

Gerson Fraga Vieira akishangilia na Kagere

Akizungyumza mara baada ya mchezo kumalizika, Gerson ambaye alimudu vizuri nafasi ya kiungo amesema kuwa hakutarajia kukutana na wimbi kubwa la mashabiki wa namna ile ambao wanashangilia wakati wote klabu yao, huku akiwaahidi makubwa msimu huu.

"Ulikuwa ni usiku wa kipekee kwenye maisha yangu, najisikia furaha sana kwa sababu hali ilivyokuwa hapa uwanja wa Taifa ni nzuri sana. Ninaomba kila wakati nipate sapoti kama hii ya mashabiki ambayo ni ya ajabu sana", amesema Gerson.

"Mashabiki watarajie mazuri maana napenda kucheza mpira na napenda kujipa changamoto mwenyewe, napenda kupigania mpira na napenda kuwa na mpira wakati wote", ameongeza.

Tamasha hilo la Simba Day lilikamilika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Power Dynamos ya Zambia, huku mshambuliaji Meddie Kagere akifunga hat-trick. Mchezo unaofuata wikiendi hii,  Simba itacheza na UD Do Songo ya Msumbiji katika mchezo wa hatua ya kwanza kuwania kufuzu makundi ya Klabu Bingwa Afrika.