
Lionel Messi
Messi alifunga magoli mawili jana usiku kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Huesca, mchezo ambao Barcelona walikuwa nyumbani katika dimba la Camp Nou, na wakaibuka na ushindi wa bao 4-1, Messi alifunga mabao hayo dakika ya 13 na 90, na mengine yalifungwa na Antoine Griezmann na Oscar Mingueza.
Baada ya kufunga magoli hayo mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 33, amefikisha mabao 21 msimu huu kwenye ligi kuu na ndio kinara wa ufungaji akimuacha Luis Suarez wa Atletico Madrid aliye nafasi ya pili kwa tofauti ya mabao 3.
Idadi hiyo ya mabao imemfanya Messi kuwa mchezaji wa kwanza kufunga magoli 20 au zaidi kwenye ligi kuu Hispania kwa msimu wa 13 mfululizo.
Na mchezo huo ulikuwa wa 767 kwa Messi akiichezea FC Barcelona na amefikia rekodi ya kucheza idadi hiyo ya michezo iliyokuwa ikishikiliwa na kiungo Xavi Hernandez.
Messi pia amefunga jumla ya mabao 27 msimu huu kwenye michuano yote katika michezo 36, lakini pia ameshaifungia FC Barcelona jumla ya mabao 661 tangu aanze kuitumikia klabu hiyo.