Jumapili , 15th Sep , 2019

Michuano ya Sprite Bball Kings imeendelea tena kwa leo katika Uwanja wa Ndani wa Taifa, kwa hatua ya robo fainali kupigwa ambapo miamba nane imeshuka dimbani kutafuta timu 4 za nusu fainali.

Robo fainali Sprite Bball Kings 2019

Katika mchezo wa kwanza kati ya KG Dallas na Water Institute umemalizika kwa KG Dallas kuibuka na ushindi wa vikapu 91 dhidi ya 84 na kuwa timu ya kwanza kufuzu nusu fainali, huku Michael Mbaga wa Water Institute akiongoza kwa kufunga jumla ya pointi 31.

Mchezo wa pili umemalizika kwa Flying Dribblers kuibuka na ushindi wa vikapu 90 dhidi ya vikapu 77 vya Dream Chasers. Mchezaji Jackson Vasco wa Flying Dribblers akiongoza kwa kufunga pointi 24 na katika mchezo wa tatu, Tamaduni imeibuka na ushindi wa vikapu 102 dhidi ya vikapu 67 vya Ukonga Hitmen. Stephano Mshana wa Tamaduni akiongoza kwa kufunga pointi 33.

Mchezo wa mwisho uliowakutanisha mabingwa watetezi Mchenga Bball Stars na TMT ( The Money Team ) umeisha kwa Mchenga kuibuka na ushindi wa vikapu 91 kwa vikapu 61 vya TMT, huku Baraka Sadick akiibuka mfungaji bora wa mchezo akifunga jumla ya  pointi 25.

Droo ya hatua ya nusu fainali inatarajia kupangwa kesho Jumatatu, Septemba 16 katika ofisi za EATV na EA Radio, katika kipindi cha Kipenga Extra, saa 6:00 Mchana.