Ijumaa , 25th Jun , 2021

Tunakupitisha katika viwanja mbalimbali vya kimichezo kwa kukupa ripoti zinazotokana na namba zenye vyanzo vya stori za kimichezo ndani yake na pia unaweza kuzisikia kila siku ya Jumatatu hadi Ijumaa saa moja na rovo asubuhi kupitia Super Breakfast ya East Africa Radio.

Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya soka ya Yanga, Fredrick Mwakalebela ambaye amerejea katika nafasi yake baada ya kuachiwa huru kutoka katika kifungo cha miaka mitano cha kutojishughulisha na soka.

6 - Ni idadi ya wiki ambazo mcheza tenis namba 5 kwa ubora duniani kwa upande wa wanaume, Dominic Thiem atakuwa anajiuguza na hii baada ya vipimo kuonesha nyota huyo amepata maumivu makali kwenye kiwiko chake yaliyompelekea kushindwa kuendelea na mchezo kwenye michuano ya Wembledon.

Matabibu pia wamesema Thiem atafungwa kiambata kwenye kiwiko chake kwa wiki hizo 6 nyingine ili kumsaidia kupunguza maumivu akiwa mchezoni.

5 - Ni idadi ya miaka aliyofungiwa Makamu Mkiti wa klabu ya Yanga, Fredrick Mwakalebela kujihusisha na soka ndani na nje ya Tanzania kwa makosa ya Uchochezi na kusema uongo juu ya mkataba wa mchezaji BM3, lakini usiku wa kuamkia leo kamati ya Maadili ya Shirikisho la mpira wa miguu nchini TFF imetangaza kumuondoa adhabu hiyo kiongozi hiyo pamoja na msamaha wa kulipa faini ya shilingi milioni 7.

Taarifa iliyotolewa na kamati hiyo imesema Mwakaleba amekiri kosa nakuomba kuuhudumia mchezo wa soka nchini na kuahidi kuwa muadilifu kwa kufuata taratibu, sheria na kanuni za mchezo huo.

4 - Ni idadi ya timu zilizoshika dimbani usiku wa kuamkia leo kutoka kundi A kwenye michuano ya COPA AMERICA ambapo timu ya Uruguay imeifunga Bolivia 2-0 kwa mabao ya Jairo Quinteros aliyejifunga dakika ya 40 na la pili likifungwa na Edinson Cavani dk79.

Chile imepokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Paraguay kwa mabao ya Braian Amaduilo dk33 na Miguel Almiron dk58 kwa penalti.

Kwa matokeo hayo, Paraguay ipo nafasi ya pili kundi B akiwa na alama 6, Chile nafasi ya tatu akiwa na alama 5, Uruguay nafasi ya nne akiwa na alama 4, Bolivia akishika mkia bila alama yeyote ilhali Argentina ikiwa kinara kwa kuwa na alama 7.

3 - Ni idadi ya mzunguko kwenye michezo ya fainali ya ligi ya mpira wa kikapu nchini Marekani NBA kwa ukanda wa Magharibi, ambapo Los Angeles Clippers bila Kawhi Leonard wamefanikiwa kuibuka na ushindi wa alama 106-96 dhidi ya timu sumbufu ya Phoenix Suns ya Chris Paul.

Paul George ndiye aliyeibeba Clippers kwenye mabega yake kwa kufikisha alama 27, rebaundi 15 na assisti 8 na kuibuka kuwa nyota wa mchezo.

Ushindi huo umefufua matumaini ya Clippers kuelekea fainali kwani walishapigwa 2-0 hivyo kwa sasa ni 2-1.

2 - Ni idadi ya siku zilizosalia kufikia tarehe 27 Juni 2021 siku ambayo klabu ya Yanga itafanya mkutano wake mkuu. Kuelekea kwenye siku hiyo inayosubiriwa na Wanayanga wengi kupaza sauti zao zao juu ya mwenendo wa timu yao,

Kaimu Khatibu Mkuu wa klabu ya Yanga, Haji Mfikirwa amesema sekretarieti imekamilisha maandalizi ya mkutano huo kwa asilimia kubwa kabisa na kuweka wazi kuwa moja ya agenda tatarijiwa ni Wanayanga kupitisha Mapendekezo ya mabadiliko ya katiba mpya ya klabu hiyo ambaye itawezesha mabadiliko ya uendeshwaji wa klabu hiyo kwenda kwenye mfumo wa kisasa.

1 - Ni idadi ya timu itakayofuzu kucheza fainali ya kombe la TFF ASFC 2020-21 itakayotoka kwenye mchezo wa nusu fainali ya kwanza itakayochezwa saa 9:30 Alasiri ya leo Juni 25, 2021 kwenye dimb la Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora ikizikutanisha timu ya Wananchi Yanga na Maafande wa mpakani klabu ya Biashara Utd Mara.

Kuelekea kwenye mchezo huo, Kocha msaidizi wa Biashara, Marwa Chamberi amesema wanaiheshimu wapinzani wao, lakini amewatahadharisha kuwa watakutana na mchezo mgumu sana kwani malengo yao ni kutinga fainali hiyo kwa namna yeyote.

Mchezo wa Nusu fainali ya pili wa kombe hilo utachezwa kesho Juni 26,2021 kwenye dimba la MajiMaji Songea mkoani Ruvuma, Mabingwa watetezi Simba watakipiga na Waoka mikate, Azam Fc saa 9:30 alasiri.