Mipango ya Ndayiragije kwenye michuano ya CHAN

Jumatano , 1st Jul , 2020

Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya soka ya Tanzania Etienne Ndayiragije amesema amepokea kwa furaha taarifa ya Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), kupanga michuano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) ifanyike Januari 2021 nchini Cameroon.

Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya soka ya Tanzania Etienne Ndayiragije akiwa amebebwa na wachezaji.

Katika mahojiano na East Africa Radio na East Africa Television leo Julai 1, 2020, Kocha huyo raia wa Burundi amesema baada ya wasiwasi kama michuano itakuwepo au haitakuwepo sasa wamepata ufafanuzi.

''Awali tulikuwa njia panda juu ya hatma ya michuano hii kama itafanyika au haitafanyika ukichukulia  tumefuzu kwa jasho sana ila sasa tuna furaha", amesema.

Kuhusu viwango vya wachezaji baada ya dharura ya Corona, amesema bado vipo juu kutokana baadhi ya mechi za ligi kuu na mashindano Azam Sports Federation Cup yanayoendeela na amefanikiwa kuyatazama.

Pia amesema kuwa muda wa mashindano ambao ni  Januari 2021, unaweza kuonekana ni mrefu lakini kiufundi ni muda mchache sana hivyo lazima waandae timu.