Jumamosi , 17th Nov , 2018

Shirikisho la soka nchini (TFF) kupitia kwa Mwenyekiti wa kamati ya Uchaguzi, Malangwe Mchungahela imesema kwamba haimtambui Yussuf Manji kama  Mwenyekiti wa Yanga kwani katiba ya timu hiyo hairuhusu mkutano mkuu kumrejesha mwenyekiti aliyejiuzulu.

Mashabiki wa Yanga wakiwa makao makuu ya klabu hiyo,.

Hatua hiyo imekuja baada ya jana jioni wajumbe wa kamati  ya utendaji ya klabu ya Yanga kukutana na mwenyekiti huyo wa kamati ya uchaguzi wakiwa na hoja ya kukubali kufanya uchaguzi katika nafasi zingine isipokuwa nafasi ya Mwenyekiti.

"Sisi kama TFF hatumtambui Manji kama mwenyekiti  wa Yanga maana alishakutana na Waziri wa Michezo,  Dk Harrison Mwakyembe ili kuzungumzia suala la  kurudi Yanga na alimkatalia'', alisema Mchungahela.

Mchungahela alisisitiza kwa mujibu wa katiba ya  Yanga, Ibara ya 28 kanuni ya tatu (kifungu kidogo c), inasema mjumbe  atakoma kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji iwapo  atashindwa kutekeleza majukumu ya mjumbe kutokana na kuumwa au sababu nyingine yoyote kwa  kipindi cha miezi 12 mfululizo.

Katiba hiyo ya marekebisho ya mwaka 2010, Ibara ya  14 inamruhusu mwanachama yoyote kujiuzulu na  kuwasilisha barua kwa katibu mkuu wa Yanga kwa barua ya rejesta. Mchungahela alisema kwa kuzingatia hilo hawamtambui Uenyekiti wa Manji.