Jumatano , 7th Oct , 2015

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha mbio za mwenge zitakazofanyika Oktoba 14 mwaka huu katika uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk,Jakaya Kikwete

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, mkuu wa mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa amesema kuwa kilele cha mbio za mwenge zitakwenda sambamba na kumbukumbu ya miaka 16 ya kifo cha baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambapo dua maalum ya kumwombea itafanyika kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere vilivyoko mjini hapa.

Amesema mwenge wa uhuru utaingia mkoani Dodoma kesho ukitokea mkoani Singida ambapo utakimbizwa katika wilaya zote saba za mkoa wa Dodoma.

Amesema mwenge huo ukiwa mkoani Dodoma utakimbizwa umbali wa kilometa 1,304.4 ambapo utazindua jumla ya miradi 39 yenye thamani ya sh, 9.8 bilion.

Aidha amesema mkoa wa Dodoma pia utatumia nafasi hiyo kumuaga Rais Kikwete katika hafla maalum iliyopangwa kufanyika katika ukumbi mpya wa CCM wa Dodoma Convention Centre uliopo kwenye barabara ya kwenda Chuo kikuu cha Dodoma (Udom).

Wakati huo huo amewataka wakazi wa mkoa wa Dodoma kufuata sheria katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 ambapo amesema kuwa mkoa umejipanga vema kwa ajili ya kukabiliana na wale wote ambao watafanya uvunjifu wa amani katika mkoa huu.