Jumamosi , 7th Dec , 2019

Kaimu Mwenyekiti wa klabu ya soka ya Simba Mwina Kaduguda, ameweka wazi kuwa mwekezaji wa klabu hiyo Mohammed Dewji ameahidi kuwapokesha Bajaj na Pikipiki mashabiki wa Simba ili waongeze kipato.

MO Dewji na John Bocco

Kaduguda ameyasema hayo leo mbele ya wanachama wa Simba waliojitokeza kwenye uwanja wa Bunju kwa lengo la kujionea baada ya awamu ya kwanza ya ujenzi kukamilila.

“Mwenyekiti wa Bodi, Mohammed Dewji ameahidi kukopesha bajaj na pikipiki ili kusaidia matawi kwa wanaopenda kujishughulisha na hilo halipo kwenye sehemu ya pesa ambayo anatoa.”- Kaimu Mwenyekiti, Mwina Kaduguda.

Kwa upande wake nahodha wa klabu hiyo John Bocco kwa niaba ya wachezaji, ameushukuru uongozi wa Simba kwa kujenga viwanja hivyo.

“Tunashukuru kwa viwanja hivi, vitatuongezea nguvu kuhakikisha tunashinda. Nawashukuru viongozi pamoja na mwekezaji, najua wamepitia vikwazo vingi lakini wameweza kufikia hii hatua. Nawashukuru mashabiki wetu kwa kujitokeza kwenye eneo hili na viwanjani au tukisafiri mikoani. Nawashukuru sana, nawaomba muendelee kuwa na upendo kwa wachezaji na viongozi.”- Nahodha.

Naye mwenyekiti mstaafu wa Simba Hassan Dalali amesema, “Kwanza namshukuru Mwenyekiti wa Bodi kwa kututengezea uwanja. Inahitaji moyo sana kufanya kazi ya kujitolea hata sisi miaka ya nyuma tulijenga majengo kwa kujitolea kwa kubeba matofali kichwani na yeye sasa anaendeleza hilo. Na sisi tunampongeza tupo nyuma yake kumuunga mkono”- Mwenyekiti Mstaafu Hassan Dalali.