Jumapili , 29th Mei , 2016

Hatimaye klabu ya soka ya Hull City imefanikiwa kutwaa ubingwa wa mchuano wa mchujo [mtoano] maarufu kama Play off baada ya kuwachapa wapinzani wao timu ya Sheffield Wednesday katika fainali iliyopigwa jana usiku.

Mohamed Diame 'Mo' akishangilia bao lake la ushindi Sheffield.

Katika mchezo huo Mshambuliaji hatari wa Hull City Mohamed Mo Diame alifunga bao safi kwa ufundi akiukwamisha mpira katika nyavu za juu ndani ya goli na kuwapa ushindi muhimu ulioipandisha Ligi Kuu ya Uingereza EPL.

Mchezaji huyo wa Kimataifa wa Senegal alipokea mpira nje ya eneo la hatari na kupenya na mpira mbele ya beki Kieran Westwood na kufunga goli hilo pekee kiufundi katika fainali hiyo iliyochezwa katika dimba la Wembley jijini London.

Kwa ushindi huo sasa Hull City ambayo ilicheza hatua ya mtoano ikiungana na vilabu vingine vilivyoshika nafasi za juu kuanzia ya tatu hadi ya sita vya Brighton & Hove Albion, Derby County na Sheffield Wednesday inapanda daraja kwenda Ligi Kuu ya Uingereza.

Na kupanda daraja kwa Hull City kunakamilisha idadi ya timu tatu zinazopanda daraja msimu ujao wa EPL ikiungana na Mabingwa wa Daraja la kwanza Championship timu ya Burnley na mshindi wa pili timu ya Middlesbrough ambazo zilipanda moja kwa moja baada ya kushika nafasi mbili za juu.

Sheffield Wednesday wao kipigo hicho kinawafanya wakose nafasi nyingine ya kurejea katika ligi kuu ya Uingereza kwa mara nyingine tangu walipofanya hivyo miaka 16 iliyopita waliposhiriki ligi hiyo kubwa.

Wakati huo huo pamoja na kuipandisha timu hiyo kocha mkuu wa klabu ya Hull City, Steve Bruce, amesema atachukuwa muda kabla ya kuangalia mustakabali wake kama kocha wa timu hiyo.

Kocha huyo mwenye miaka 55 amesema atafanya maamuzi baada ya kuhakikishiwa mambo muhimu ya kuifanya timu hiyo kwenda kushindana katika EPL katika mlengo sahihi.

"Amesema anaendelea kusikia habari nyingi juu ya kuna uwezekano timu hiyo ikanunuliwa na anachosubiri ni kujua juu ya hatma ya suala hilo kwanza".

Timu imekuwa sokoni kwa muda mrefu tangu mnamo mwaka 2014, hii ni baada ya chama cha Soka Uingereza FA kumsimamisha aliyekuwa mmiliki wake Assem Allam kufuatia kutaka timu hiyo kubadilishwa jina na kuwa Hull Tigers.