Jumapili , 21st Apr , 2019

Kufuatia kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera kulalamikia maamuzi ya waamuzi katika mchezo ambao Yanga ilipoteza dhidi ya Mtibwa Sugar, uongozi wa klabu ya Mtibwa umeibuka na kupinga vikali malalamiko hayo. 

Kifaru

Kikosi cha Mtibwa Sugar kilifanikiwa kuibuka kidedea mbele ya Yanga kwa ushindi wa bao 1-0, Jumatano, April 17 katika uwanja wa Jamhuri Morogoro, ambapo baada ya mchezo, kocha wa Yanga alionesha kutofurahishwa na maamuzi ya waamuzi waliochezesha mchezo huo. 

Uongozi wa Mtibwa Sugar kupitia kwa Afisa Habari, Thobias Kifaru umesema kuwa unashangazwa na taarifa zinazoelezwa kwamba wamebebwa ilihali mpira ulikuwa wazi na kila mmoja amaeona kilichotokea.

"Niliwaambia mapema ndugu zangu wa Yanga kwamba hapa ni lazima tuwachape kama ambavyo wao walifanya kwao, hicho ndicho kilichotokea na tumebeba pointi tatu, nashangaa wanadai tumebebwa wakati tuliwazidi mbinu na juhudi uwanjani wapinzani wetu wanapaswa wajipange", amesema Kifaru.

"Kinachowauma Yanga najua wanaona Mtibwa tumewapunguzia kasi na nguvu ya kuendelea kubaki kileleni ila nasi hatukuwa na namna maana tunataka tuwe ndani ya timu tatu bora sasa hatuwezi kufika hapo kama tutafungwa kiwepesi, tunajiamini na tunapambana kwa kila anayefuata hapa ni lazima tumyooshe," ameongeza.

Mtibwa Sugar imecheza michezo 32 imejikusanyia pointi 48 ikiwa nafasi ya nne imeshinda michezo 14, sare 6 na imepoteza michezo 12.