Jumamosi , 9th Jul , 2016

Hatimaye baada ya kubana kwa muda mrefu usajili wa mshambuliaji mwenye kasi Shiza Kichuya uongozi wa mabingwa wa zamani wa soka Tanzania bara misimu miwili ya mwaka 1999 na 2000 timu ya Mtibwa ya Morogoro wamemruhusu kinda huyo kutua Simba msimu huu

kiungo wa mshambuliaji wa pembeni wa Mtibwa Shizza Ramadhani Kichuya.

Unaweza kusema suala la usajili baina ya wekundu wa Msimbazi na kiungo wa mshambuliaji wa pembeni wa Mtibwa Shizza Ramadhani Kichuya liko safi kwa asilimia 99 mara baada ya pande zote mbili kuafikiana kufanya kazi pamoja kwa miaka miwili ijayo.

Shizza mwenyewe amesema baada ya viongozi wake kumpa baraka zote na ridhaa kufanya mazungumzo na Simba SC alifika jijini Dar es Salaam na kumalizana na timu hiyo rasmi na wakati wowote mchezaji huyo mwenye nguvu na kasi atamwaga wino na kujiunga na timu hiyo ambayo inataraji kuweka kambi mjini Morogoro kujiwinda na msimu mpya wa michuano ya Ligi Kuu na michuano mengine ijayo.

Kichuya awali alikuwa anasuasua kufanya maongezi ya moja kwa moja na timu ya Simba hasa kutokana na taratibu za mikataba kumbana ikumbukwe mchezaji huyo ambaye ni moja wa wachezaji wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa ligi kuu msimu huu amebakiza mwaka mmoja katika Mkataba wake na Mtibwa, ambao ni mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara mara mbili mfululizo,msimu wa mwaka 1999 na 2000.

Aidha hii leo Julai 9 msemaji wa klabu ya Mtibwa Thobias Kifaru Lugalambwike ameithibitishia East Afrika Radio kuwa mchezaji Kichuya ni mali halali ya Simba na wao kama timu wameridhia mchezaji huyo kwenda kupata changamoto mpya hii ni baada ya mchezaji mwenyewe kuonyesha nia na hitaji la kutua katika klabu ya Simba.

Simba kwa sasa itakuwa chini ya mkufunzi mpya raia wa Cameroon Joseph Omog akisaidiwa na kocha Jackson Mayanja raia wa Uganda/

Na Kama mchezaji huyo atasaini Simba, basi atakuwa mchezaji wa tatu wa Mtibwa kuhamia Simba SC majira haya baada ya awali Simba kunasa saini ya viungo wa timu huyo Muzamil Yassin na Mohamed ‘Mo’ Ibrahim.