Jumanne , 13th Nov , 2018

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amezungumzia juu ya taarifa ya Baraza la Wadhamini kuweka hadharani barua rasmi ya Yusuf Manji inayoonesha kurejea kwenye nafasi yake ya Mwenyekiti, jambo lililozua sintofahamu baina ya TFF na klabu.

Dkt.Harrison Mwakyembe

Katika taarifa yake, Waziri Mwakyembe amesema kuwa serikali haitobadili utaratibu wake kama ulivyotangazwa na TFF, kwamba uchaguzi ni lazima ufanyike ili kuwapata viongozi wapya wa kuchaguliwa.

"Yeyote mwenye nia ya kugombea katika uchaguzi akiwemo Yussuph Manji, ni vema wamshawishi achukue fomu ili kuthibitisha kweli yeye ni kiongozi anayependwa na wote, sio hizi njia za mkato ambazo vyombo halali vinaweka sheria lakini zinataka zivunjwe," amesema.

"Mimi sisikilizi maneno mitaani na kama serikali itakuwa inaambiwa 'kijiwe' kimesema hivi halafu tukaanza kuitikia hapo basi kutakuwa na matatizo makubwa, fuatilieni TFF wanasema nini halafu waulizeni BMT wanasemaje, baadaye BMT wataniletea mimi," ameongeza Mwakyembe.

Aidha Mwakyembe amesema kuwa kiongozi huyo alifuatwa mara kadhaa ili kurejea katika nafasi hiyo akiwemo yeye mwenyewe ambaye alimfuata mara tatu lakini alikataa, akishangaa urejeo wake hivi sasa ikiwa imeshapita zaidi ya miezi mitano.

TFF iliiagiza Yanga kufanya uchaguzi wake haraka iwezekanavyo, jambo ambalo limeleta mtafaruku kwa wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kutokana na wengi kutokubaliana na suala la usimamizi wa uchaguzi huo, wakitaka usimamiwe na kamati ya uchaguzi ya klabu bila kuingiliwa na TFF.