Jumamosi , 16th Jul , 2016

Kiungo mkabaji wa Leicester City N’Golo Kante amesaini mkataba wa miaka mitano kujiunga na matajiri wa London, Chelsea.

N'Golo Kante

Kante ambaye alikuwa nguzo muhimu ya ubingwa wa Leicester City msimu uliopita, amejiunga na Chelsea kwa dau la Paund milioni 30.
Kiungo huyo kisiki, alijiunga na mabingwa hao msimu uliopita akitokea Caen kwa dau la paund million 6.

Ameichezea Leicester mechi 40 na kufanikiwa kutwaa kombe la ligi kuu nchini England msimu wa 2015/16.

Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 25 alikuwa ni sehemu kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa kilichoshiriki michuano ya Euro 2016 na kufanikiwa kufika hatua ya fainali.

Akielezea furaha yake, Kante amesema “Nina furaha sana kujiunga na moja ya klabu kubwa barani Ulaya na duniani, hii ilikuwa ni ndoto yangu na sasa imekuwa kweli”

Aliongeza pia “Fursa ya kufanya kazi na kocha Antonio Conte ambaye ni miongoni mwa makocha bora duniani, pamoja na baadhi ya wachezaji wa kiwango cha juu, ilikuwa ni kishawishi kikubwa kwangu kukubali kusaini Chelsea”

Kante ni mchezaji wa pili kusainiwa na Chelsea kuelekea msimu ujao, baada ya mshambuliaji raia wa Ubelgiji Michy Batshuayi aliyejiunga na timu hiyo kutoka Marseille ya Ufaransa