Alhamisi , 18th Feb , 2016

Klabu ya Ngome ya mchezo wa Mieleka inayojiandaa kushiriki mashindano ya wazi ya kitaifa na ya kimataifa imesema licha ya kuwa na wachezaji wachache ina uhakika wa kuchukua ubingwa katika mashindano hayo.

Kocha wa timu hiyo Henry Mrisho amesema, mashindano yaliyo mbele yao ni makubwa na wachezaji wengine wapo katika kikosi cha timu ya taifa wakijiandaa katika mashindano ya kuwania kufuzu olimpiki mwaka huu ambapo kikosi kilichobaki ni cha wachezaji wachache ambao wanajipanga kwa ajili ya kuweza kuibuka na ushindi.

Mrisho amesema, mashindano ya wazi yataongeza hamasa zaidi kwa wachezaji kuonesha uwezo wao kwani kutakuwa na mchujo wa kuweza kuchagua wachezaji wengine wazuri zaidi ambao wataweza kuungana na kikosi cha timu ya taifa.

Mrisho amesema, bado wanaendelea kuhamasisha mikoa mingine kuweza kuwa na vilabu mbalimbali kwa kufanyia mashindano mikoani, kuandaa vilabu vya mitaani ambavyo huwa vinashiriki katika mashindano ya wazi ili kuweza kuinua vilabu vidogovidogo pamoja na kuandaa timu mbalimbali za mikoani ili kuweza kushiriki mashindano ya wazi ya mwaka huu.