Ijumaa , 10th Jun , 2016

Shirikisho la ngumi za ridhaa nchini Tanzania BFT sasa limethibitisha rasmi kuwa kati ya michuano miwili iliyosalia ya kufuzu kwa Olimpiki watashiriki mchuano mmoja pekee ambao utafanyika nchini Venezuela mwanzoni mwa mwezi wa saba mwaka huu.

Baadhi ya mabondia wa timu ya taifa wakiwa katika mazoezi.

Timu ya taifa ya ngumi za ridhaa sasa inataraji kushiriki shindano moja tu la mchujo lililobaki kati ya mawili ili kusaka tiketi ya kushiriki mashindano ya Olimpiki ya Rio Brazil yatakayoanza mwanzoni mwa mwezi Agasti mwaka huu.

Makamu wa rais wa shirikisho la ngumi Tanzania BFT Lukelo Wililo amesema awali walikuwa washiriki pia mashindano ya Azabeijan ambayo yatafanyika katikati ya mwezi huu wa Juni lakini sasa wameona washiriki ya Venezuela yatakayofanyika mapema mwezi Julai mwaka huu.

Wililo amesema kutokana na hali ya kifedha kuwa mbaya ndani ya shirikisho [BFT] wameona bora wachague ya Venezuela ambayo yako mbali kidogo jambo ambalo litawasaidia wao kujipanga na pia timu kufanya maandalizi ya kutosha zaidi.

Aidha Wililo amesema mashindano hayo ya kufuzu ya huko Venezuela ambayo ni ya mwisho kabisa kwa mabondia kote duniani kusaka fursa hiyo ya kufuzu yatahusisha pia mabondia wa ngumi za kulipwa hii ni kufuatia mabadiliko ya kanuni yaliyofanyika hivi karibuni yakihusisha shirikisho la ngumi la kimataifa AIBA na wadau na wanachama na mashirikisho shiriki ya ngumi kote Ulimwenguni na kufikia azimio hilo.

Akimalizia Wililo amesema mpaka sasa ni Thomas Mashali ndiye bondia pekee wa ngumi za kulipwa nchini aliyejiandikisha na wao kama BFT wameshamfanyia taratibu zote za kwenda kushiriki michuano hiyo na kimsingi anatoa wito kwa Serikali, wadau na makampuni kulisaidia shirikisho la ngumi nchini [BFT] kufanikisha maandalizi na hatimaye safari ya timu hiyo kwenda kushiriki michuano ya mchujo na baadae Olimpiki yenyewe kwa wale watakaofuzu.

Pia Wililo amewataka mabondia wenye uwezo wa ngumi za kulipwa nchini kujitokeza kutumia fursa hiyo ili kuliletea sifa Taifa lakini pia kujitangaza wao wenyewe pia katika medani ya kimataifa na kukuza uchumi wao binafsi.