Jumatatu , 30th Jul , 2018

Mchezaji kutoka timu ya Kikapu ya Portland inayoshiriki michuano ya Sprirte Bball Kings Ally Atiki ameondoka leo Julai 29, kuelekea nchini Afrika Kusini kushiriki kambi ya mafunzo ya mchezo huo, inayojulikana kama Basketball Without Borders (BWB).

Kikosi cha Portland na aliyewekewa kiboma chekundu ndio Ally Atiki

Kambi hiyo itakayofanyika jijini Pretoria itaanza Jumatano Agosti 1 na kukamilika Agosti 4 na itaendeshwa na wachezaji wa Kikapu kutoka mataifa ya Ulaya na Marekani wanaocheza ligi ya Kikapu ya Marekani.

Katika safari hiyo Atiki pia ataambatana na mchezaji wa kike wa Kikapu Jesca Ngisaise Onga'anyi, Kocha wa timu ya Taifa ya Vijana Bahati Mgunda na viongozi wa Shirikisho la Kikapu nchini (TBF) Rais Phares Magesa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es salaam (BD) Okare Emesu.

Mbali na kambi hiyo, pia kutakuwa na mchezo wa NBA Africa 2018, ambao utakutanisha timu za Team Africa dhidi ya Team World, na utafanyika August 4 saa 11 jioni, Sun Arena, Time Square.

Ally Atiki jana Julai 29, alikuwa dimbani kwenye uwanja wa taifa wa ndani na timu yake ya Portland kwenye mchezo wa nusu fainali ya kwanza kati ya tatu za 'Best of three' ambapo timu yake ilikubali kichapo cha pointi 70 kwa 54. 

Mechi za pili za nusu fainali zitapigwa Jumamosi ijayo Agosti 4 kwenye uwanja wa taifa wa ndani ambapo Flying Dribblers wanahitaji ushindi tu dhidi ya Team Kiza ili kutinga hatua ya fainali baada ya kushinda mechi ya kwanza kwa pointi 84 kwa 75.