Jumatatu , 6th Dec , 2021

Uongozi wa Mtibwa Sugar umesema hauna mpango wa kuachana na Kocha wao kutoka nchini Cameroon Joseph Omog, licha ya kuanza vibaya majukumu yake msimu huu 2021/22.

Kocha mkuu wa Mtibwa Sugar (Kushoto) akiteta jambo na msaidizi wake Awadh Issa.

Mtibwa Sugar imeshindwa kupata alama tatu katika michezo saba ya Ligi Kuu Tanzania Bara waliocheza hadi sasa, jambo ambalo liliibua sintofahamu kwa wadau wa soka nchini kwa kuhusu huenda kocha Omog akaondolewa kwenye nafasi yake.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru amesema bado Uongozi una imani na Kocha huyo, ambaye aliwahi kuvinoa vikosi vya Simba SC na Azam FC kwa nyakati tofauti.

Amesema wanaheshimu misingi ya Mkataba uliopo kati yao na Kocha Omog na wanaamini atafanikisha lengo la kuirejesha Mtibwa Sugar kwenye Reli ya ushindi kama ilivyowahi kuwa siku za nyuma.

“Tuna mkataba na Joseph Omog wa miaka miwili, hivyo tutaendelea kuwa naye, tunaamini huu ni upepo mbaya tu na utapita na hali itakuwa sawa tu,”

“Omog ni kocha mkubwa na mwenye rekodi za aina yake. Kumbuka yeye ndiye alikuwa kocha mzawa pekee wakati anaiongoza nchi yake Cameroon kwenye michuano ya Afcon iliyopita hivyo tuna imani naye,” amesema Kifaru.

Mtibwa Sugar inaburuza mkia wa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa imeshacheza michezo saba, imepata sare katika michezo miwili, imepoteza kwenye michezo mitano na haijashinda mchezo wowote hadi sasa.