Jumatatu , 21st Jan , 2019

Tunaendelea kukuletea majibu ya baadhi ya maswali magumu aliyoulizwa kocha wa zamani wa Chelsea na Manchester United, Jose Mourinho, ambayo yatakusaidia kumtambua vizuri zaidi kwa maana ya falsafa zake anazoziamini na namna anavyojipima katika ulimwengu wa soka.

Jose Mourinho

Aliulizwa maswali hayo na kuyajibu wakati akifanya uchambuzi wa mechi za michuano ya bara la Asia pamoja na baadhi ya michezo ya Ligi Kuu nchini Ungereza ( EPL) katika televisheni ya Bein Sports wikiendi iliyopita.

Hii hapa ni sehemu ya pili ya maswali magumu ambayo Mourinho ameulizwa na kutoa majibu yake.

Jinsi alivyofanikiwa kutoka kuwa kocha wa chini ambaye hakuwahi kucheza mpira ngazi ya juu, hadi kuwa kocha bora Duniani.

Mourinho: "yawezekana watu hawanifahamu vizuri mimi kama binadamu, mimi ni aina ya mtu ambaye sina muonekano mzuri ninapoonekana katika televisheni au mazingira yangu ya kazi. Nafikiri kuwa sifananii kuwa katika jamii ya mpira, nimekuwa katika mpira tangu utotoni, sina muda wa kupoteza kutengeneza wadhifa au sifa kwa jamii. Kila kitu nilichonacho ni kutokana na kufuatilia kazi zangu na matokeo, hakuna alienipa chochote".

"Nimekuwa kocha bora Duniani bila kuwa mchezaji mkubwa, nimevunja kuta zote zilizokuwepo wakati huo".

Anachukuliaje jinsi yeye anavyochukuliwa dhidi ya makocha wengine pindi wanapokosea?

Mourinho: "watu muda mwingine wanachanganya kati ya utashi na kuzuia hisia, tukio linaweza kuwa sawa kwa makocha wengine, lakini matokeo yake yanakuwa tofauti kwangu. Pale Mourinho anapofanya kosa uwanjani, pale Mourinho anapopiga chupa, anatolewa nje, anasimamishwa, lakini Jurgen Klopp au Pep Guardiola wanapofanya hivyo, inachukuliwa kama ni utashi".

Anazungumziaje ukosoaji anaopewa juu ya mfumo wake wa kupaki basi?

Mourinho: "umiliki wa mpira ni muhimu uwanjani hasa pale unapoluwa na mpira, nafikiri wengi wanajua kuwa Chelsea si wazuri hasa wanapokuwa bila mpira kwahiyo ni rahisi kuwadhibiti wasipokuwa na mpira kwahiyo ni rahisi pia kuwadhuru, mchezo wa soka ni wa mipango. Malalamiko ya kupaki basi nakumbuka yalianza pindi nikiwa Real Madrid, pale ambapo tulikuwa mabingwa kwa pointi 100 na magoli 116 na watu wakawa wanajiuliza inawezekanaje hilo".

Ni timu gani anaipa nafasi ya kubeba ubingwa wa EPL msimu huu na namna timu nne za juu zitakavyokuwa?

Mourinho: "nafikiri katika nafasi ya kwanza na ya pili ziko wazi, tangu mwanzo wa ligi na hata mpaka sasa timu zilizopo juu, Liverpool na Manchester City ndizo zitakazoamua mshindi lakini nafasi ya tatu, ya nne na tano ndipo ugumu ulipo, kwani ni timu ambazo zinabadilika kuanzia Desemba hadi mwishoni mwa ligi".