
Kocha huyo raia wa Uholanzi amewahi kupata mafanikio makubwa akiwa na mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara Yanga SC ambapo alifanikiwa kutwaa ubingwa wa VPL kwa misimu miwili mfululizo.
Huwezi kutaja mafanikio ya Yanga ya kutwaa ubingwa mara tatu mfululizo katika miaka ya hivi karibuni bila kumtaja Pluijm. Alianza kushinda msimu wa 2014/15 kabla ya kutwaa tena 2015/16. Zaidi ya VPL Pluijm ndio alikuwa kocha wa kwanza kutwaa kombe la shirikisho (FA) msimu wa 2015/16.
Alianza vizuri msimu wa 2016/17 akiwa na Yanga kabla ya kuondolewa kwenye nafasi ya ukocha mkuu na kukabidhiwa nafasi ya kuwa Mkurugenzi wa ufundi na nafasi yake kuchukuliwa na Mzambia George Lwandamina lakini hakudumu na nafasi hiyo ambapo aliachana na timu hiyo na kuteuliwa rasmi kuwa kocha wa Singida United ambayo imepanda ligi msimu huu wa 2017/18.
Mholanzi huyo amejiwekea rekodi nzuri ndani ya Singida United msimu huu akiwa amepoteza mechi moja tu kati ya 12 alizoiongoza timu hiyo kwenye VPL. Katika michezo hiyo Pluijm ameshinda mechi 6 na kutoka sare mechi 5.
Pluijm ameisadia Singida United kuleta ushindani mkubwa kwenye ligi tofauti na vilabu vingine ambavyo huwa vinapanda daraja. Hadi sasa SIngida United inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama 23. Lakini pia imefuzu hatua ya 32 ya kombe la FA. Jana pia Pluijm ameiongoza Singida United kushinda 3-2, mchezo wake wa kwanza wa Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar dhidi Zimamoto.