Jumapili , 29th Jul , 2018

Timu nne zilizofuzu hatua ya nusu fainali ya Sprite Bball Kings leo Julai 29, 2018 zinashuka dimbani kucheza mechi za kwanza kati ya zile tatu za kuamua ni timu gani zinakwenda hatua ya fainali huku kukiwa na timu mbili zilizofika hatua hii kwa mara ya pili.

Team Kiza wenye jezi nyeupe walipocheza na DMI waliovaa nyeusi kwenye mechi ya robo fainali.

Katika mechi hizo zitakazopigwa kwenye uwanja wa taifa wa ndani, mechi ya kwanza itakuwa ni kati ya timu iliyocheza nusu fainali 2017, Flying Dribblers dhidi ya wageni wa hatua hii Team Kiza huku mechi ya pili ikiwa ni wageni wengine wa nusu fainali, timu ya Portland wakiwakaribisha mabingwa watetezi Mchenga Bball Stars.

Flying Dribblers wanacheza nusu fainali yao ya pili mfululizo wakiwa na kumbukumbu ya kutolewa na Mchenga Bball Stars mwaka 2017, ambao walikwenda kuwa mabingwa. Mwaka huu wamefanikiwa kufika hatua hii tena.

Portland wao waliishia hatua ya mchujo kwa mwaka 2017 lakini mwaka huu wamejipanga vyema wakiwa ndio timu iliyofunga pointi nyingi zaidi (257) tangu mashindano yaanze. Leo watakuwa na kibarua wakiikabili Mchenga Bball Stars ambao katika mechi mbili tu wamefunga pointi 201.

Kwa mujibu wa kamati ya maandalizi kutoka East Africa Televison kwa kushirikiana na shirikisho la Kikapu nchini (TBF), maandalizi yamekamilika na mechi zitaanza saa 10:00 jioni. Mechi za nusu fainali zinacheza kwa mtindo wa 'Best of three', lakini ikitokea timu moja ikashinda mechi 2 za kwanza itakuwa imefuzu hatua ya fainali bila kucheza mechi ya tatu.

Sprite Bball Kings inadhaminiwa na kinywaji baridi cha Sprite na mshindi ataondoka na kitita cha shilingi milioni 10, mshindi wa pili milioni 3 na mchezaji bora 'MVP' akiondoka na shilingi milioni 2.