Jumatano , 9th Mei , 2018

Rais wa shirikisho la soka nchini (TFF) Wallece Karia amesema mlinda mlango wa Yanga na timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 20 Ngorongoro Heroes Ramadhani Kabwili amesharejea kwenye kambi ya timu hiyo.

Ramadhani Kabwili ameungana na wachezaji wenzake kambini baada ya utata kati ya klabu yake ya Yanga na kocha Ammy Ninje kumalizwa na Rais Karia hivyo sasa mambo yapo kama kawaida.

''Kabwili ameshajiunga na wenzie kambini na kilichotokea mpaka Kabwili kwenda nchini Algeria kuitumikia timu yake ya Yanga kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya U.S.M Alger ni kutokuwa na mawasiliano mazuri kati ya uongozi wa TFF na uongozi wa Klabu ya Yanga'', amesema.

Awali kocha wa Ngorongoro Heroes Ammy Ninje alimwondoa Kabwili kikosini na kumwita mlinda mlango wa Peter Doto Mashauri wa Black Sailor ya Zanzibar kiziba nafasi yake. 

Ngorongoro Heroes itacheza na timu ya Taifa ya Mali U20 Jumapili Mei 13, 2018 Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kwenye mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20.