Jumamosi , 1st Nov , 2014

Kuzinduliwa kwa kituo cha michezo jijini Dar es Salaam na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete ni mwanzo mpya soka la Tanzania kufungua njia ya kuelekea kilele cha mafanikio kwa kuzalisha wachezaji wengi vijana siku zijazo

Rais ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete hii leo ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa kituo cha kukuza michezo kitakachojengwa jijini Dar es salaam maeneo ya mnazi mmoja kidongo chekundu

Ujenzi wa kituo hicho kitakachokuwa kikikuza vijana wadogo katika michezo ya mpira wa kikapu na soka unadhaminiwa kwa ushirikiano wa karibu baina ya klabu ya ligi kuu ya Uingereza Sunderland na kampuni ya Symbion Power.

Akizungumza hii leo wakati wa uzinduzi wa ujenzi huo Rais Kikwete amezungumza mambo mengi hasa ustawi wa soka la vijana hapa nchini kwani ndio mkombozi wa soka katika nchi zote kote duniani

Rais Kikwete pia amelitaka shirikisho la soka nchini Tanzania TFF kuwa wabunifu na kujitafutia vyanzo vingine vya mapato badala ya kutegemea mapato ya wadhamini wa vilabu na pesa za milangoni [viingilio- gate collection] na kuachana kabisa na hali hiyo ambayo sasa imeibua mgogoro mkubwa ambao sasa unapelekea mvutano baina ya TFF na vilabu.

Aidha Rais Kikwete akaenda mbali zaidi na kuitaka TFF kuweka sheria kali kwa vilabu hasa vya ligi kuu ambavyo vitakuwa havina timu za kudumu za vijana zisishiriki ligi kuu na pia Rais Kikwete akasema japo hali ya vilabu si nzuri lakini umefika wakati sasa kwa soka la Tanzania kuweka sheria kali kwa vilabu hasa vya ligi kuu kuwa na timu za vijana na pia kumiliki viwanja kama ilivyo kwa nchi nyingi barani ulaya kama Uingereza na Uhispania

Naye Rais wa TFF Jamal Malinzi amepongeza ujenzi huo na kusema ni fursa sasa kwa wadau wengine nao kuunga mkono juhudi hizo kwakujenga vituo kama hivyo na mikoani.

Malinzi amesema shirikisho la soka nchini TFF limejipanga katika kukuza soka kwa vijana na tayari kuna mashindano makubwa ya taifa kwa vijana chini ya miaka 13 ambayo yatasaidia kupata kikosi bora kitakachoshiriki michuano ya vijana Afrika AFCON mwaka 2019.