Ijumaa , 13th Jul , 2018

Mashindano ya mpira wa Kikapu nchini ya Sprite Bball Kings yanayoandaliwa na East Africa Television LTD kwa udhamini wa kinywaji cha Sprite, yapo katika hatua ya robo fainali na sasa rasmi mechi 4 za hatua hiyo zitapigwa kwenye uwanja wa ndani wa taifa.

Timu ya Water Institute ambayo itacheza na Flying Dribblers kwenye robo fainali.

Baada ya droo ya mechi za robo fainali kufanyika na kupangiwa tarehe ya kuchezwa ambayo ni Jumamosi Julai 21, kamati ya maandalizi imeweka wazi kuwa uwanja utakaotumika ni wa ndani wa taifa huku mechi zikianza mishale ya saa 6:00 mchana hadi 2:00 usiku. Pia hakutakuwa na kiingilio, zaidi burudani na zawadi mbalimbali kwa mashabiki zitatolewa.

Mechi 4 za hatua ya robo fainali ni kati ya Temeke Heroes Vs Portland, Mchenga Bball Stars Vs St. Joseph, Team Kiza Vs DMI, Water Institute Vs Flying Dribblers. Bingwa wa michuano hii atajinyakulia shilingi milioni 10, mshindi wa pili milioni 3 huku MVP wa mashindano ataweka mfukoni kiasi cha milioni 2.

Mechi za hatua ya mchujo pamoja na zile za 16 bora zilipigwa kwenye viwanja tofauti tofauti. Mechi 25 za hatua ya mchujo zilipigwa kwenye uwanja wa JK Park na kufanikiwa kutoa timu 15 ambazo ziliungana na bingwa mtetezi Mchenga Bball Kings katika hatua ya 16 bora.

Katika hatua ya 16 bora, mechi 4 za kwanza zilipigwa kwenye viwanja vya Airwing Ukonga, ambapo zilipatikana timu 4 zilizoingia robo fainali. Mechi 4 za pili katika hatua hiyo zilipigwa kwenye uwanja wa Bandari Kurasini na kutoa timu zingine 4 kukamilisha timu 8 za robo fainali.