
Mshambuliaji wa klabu ya Azam, Prince Dube.
Dube na Kangwa watakosekana kutokana na kuoneshwa kadi za njano tatu mfululizo hivyo kutumikia adhabu ya kukosa mchezo mmoja ambao utapigwa kwenye dimba la Jamhuri jijini Dodoma.
(Bruce kangwa (kulia) akiitumikia Azam kwenye moja ya mchezo wa Mapinduzi Cup 2021.)
Wawili hao walioneshwa kadi hizo kwenye mchezo wao uliopita dhidi ya Mtibwa Sukari ambao Dube alifunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 2-0 huku kangwa akionesha kiwango safi.
Kocha msaidizi wa matajiri hao wa Temeke, Bahati Vivier, amesema maandalizi ya mchezo huo yamekamilika na wamejiandaa vizuri kuziba nafasi za nyota hao kwani anayo imani kubwa na wachezaji wengi waliopo kikosini hapo.
Nae kocha wa JKT Tanzania, Mohamed Abdallah Bares, amesema anachosubiri ni kuona mchezo wenye ushindani mkali kutokana na ubora wa mpinzani wake huku akijigamba wachezaji wataonesha kiwango cha juu.
Dube kafikisha mabao 10 mpaka hivi sasa bao moja nyuma ya kinara wa upatikanaji mabao hivi sasa kwenye ligi kuu bara, Mnyarwanda, Meddie Kagere mshambuliaji wa klabu ya mabingwa watetezi, Wekundu wa Msimbazi, Simba mwenye mabao 11.
Wenyeji wa mchezo huo, klabu ya JKT Tanzania ipo nafasi ya 13 ikiwa na alama 27 baada ya michezo 25 ilhali Azam ipo nafasi ya tatu ikiwa na alama 47 utofauti wa alama 4 na kinara Yanga huku Simba akiwa wapili akiwa na alama 46 na utofauti wa michezo 3 nyuma ya Yanga.