Jumamosi , 7th Mei , 2016

Nyota wa Tanzania anayekipiga katika ligi kuu ya Ubelgiji Mbwana Ally Samatta maarufu kama Samagoal imeendelea kung'ara nchini humo baada ya kinda huyo mwenye kipaji kuendelea kuonesha kiwango bora kila mara anaposhuka dimbani katika ligi hiyo.

Mbwana Samatta wa Genk akimtoka beki wa Zulte Waregem.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amecheza kwa kiwango cha juu jana usiku wakati timu yake ya KRC Genk ikishinda mabao 2-0 dhidi ya Zulte Waregem katika mchezo wa Ligi ya mchujo Ubelgiji kufuzu michuano ya Ulaya.

Nahodha huyo wa Taifa Stars amecheza kwa dakika zote 90 kwa kiwango cha kumfurahisha yeyote katika mchezo huo wa nyumbani, uliopigwa katika Uwanja wa Cristal Arena mjini Genk.

Shukrani kwao, wafungaji wa mabao hayo kiungo Mkongo mzaliwa wa Ufaransa, Neeskens Kebano dakika ya 47 na beki Mnigeria, Onyinye Wilfred Ndidi kunako dakika ya 63.

Samatta amefanikiwa kuifuta kadi ya njano aliyopewa mwishoni mwa wiki iliyopita wakati KRC Genk ikifungwa mabao 3-1 na Club Brugge katika mfululizo wa michuano hiyo Uwanja wa Jan Breydelstadion mjini Brugge.

Kwa mchezo huo wa jana usiku sasa jana inamaanisha kuwa Samatta amecheza mechi ya 13 tangu ajiunge na Genk akitoka kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika na TP Mazembe pamoja na kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora anayecheza Afrika.

Katika mechi hizo, ambazo sita pekee ndiyo ameanza tangu mwanzo katika kikosi cha kwanza, mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba SC ya Dar es Salaam, amefunga mabao manne, moja katika kila mechi ambazo Genk ikishindia 2-1 ugenini dhidi ya wenyeji SV Zulte-Waregem, 4-0 na 4-1 dhidi ya KV Oostende na 3-2 dhidi ya Club Brugge mchezo wa kwanza wa play offs.