Samatta ashukuru Mungu Villa kubaki EPL

Jumatatu , 27th Jul , 2020

Mshambuliaji wa Aston Villa Mbwana Samatta amesema anamshukuru Mungu kufuatia klabu yake kubaki kwenye ligi kuu ya soka nchini Uingereza.

Mbwana Samatta

Mshambuliaji wa Aston Villa Mbwana Samatta amesema anamshukuru Mungu kufuatia klabu yake kubaki kwenye ligi kuu ya soka nchini Uingereza.

Nahodha huyo wa timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars, alianza kwenye kikosi cha Villa kilichojinasua kushuka daraja baada ya kupata sare 1-1 na West Ham Jumapili iliyopita.

Sare hiyo imeifanya Villa kumaliza nafasi ya 17 ikizizidi alama 1 Watford na Bournemouth ambao wameungana na Norwich kushuka daraja.

''Narudisha shukrani kwa Mungu kwa kuamua niendelee kubaki kwenye ligi kuu ya England tena mwakani. Asanteni kwa wote mlioniombea kheri Villa ili muendelee kuniona tena ktk ligi hii pendwa. '' Aliandika Samatta kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii.

Samatta alijiunga na Villa kwenye uhamisho wa dirisha dogo mwezi Januari mwaka huu akitokea klabu ya KRC Genk ya ligi kuu nchini Ubelgiji.

Samatta mwenye umri wa miaka 27, hakuwa na kipindi kizuri kwa nusu msimu huu aliojiunga na klabu hiyo akifunga mara moja tu katika mechi 14 za EPL, lakini huenda akawa na kazi nzuri ya kufunga kwenye msimu ujao kama alivyokuwa kwenye ligi kuu ya Ubelgiji.

Samatta amefunga jumla ya mabao 44 katika mechi 101 alipokuwa na Genk kwa miaka minne aliyokaa na Mabingwa hao wa Ubelgiji.