Alhamisi , 28th Jul , 2022

Timu ya taifa ya wanawake chini ya miaka 17 ya Tanzania ‘Serengeti Girls’ imepangwa kuanza na Japan kwenye michuano ya Kombe la Dunia, itakayoanza Oktoba 11, mwaka huu nchini India.

Timu ya taifa ya wanawake chini ya miaka 17 ‘Serengeti Girls’

Serengeti Girls imepangwa kundi D na itacheza na Japan Oktoba 12 kwenye Uwanja wa Pardit Jawaharlal, jijini Nehru.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) Morocco itacheza mechi ya ufunguzi dhidi ya Brazil kwenye Uwanja wa Kalinga Oktoba 11.

Serengeti Gils ambayo tayari imeingia kambini kujiandaa na michuano hiyo, itacheza mchezo wa pili Oktoba 15 dhidi ya Ufaransa kabla ya Oktoba 18 kumaliza dhidi ya Canada kwenye Uwanja wa DY Patil.

Tanzania sasa imeungana na Morocco na Nigeria kuiwakilisha Afrika na kukamilisha idadi ya timu 16 zitakazoshiriki fainali hizo za Dunia kati ya Oktoba 11-30 mwaka huu katika miji mitatu ya India zikiwa ni fainali za saba tangu michuano hiyo ilipoasisiwa mwaka 2008.

Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kufuzu fainali hizo kwa timu za soka. Hadi kufuzu, Serengeti ilizing’oa Botswana, Burundi na kumalizia kwa kuitoa Cameroon baada ya kuibuka na ushindi wa jumla wa mabao 5-1.