Jumatatu , 3rd Oct , 2022

Kocha mkuu wa muda wa Simba SC Juma Mgunda amesema kikosi chake bado hakina ubora anaoutaka, lakini ameweka wazi kuwa timu hiyo inapiga hatua. Simba SC inaongoza Ligi ikiwa na alama 13 katika michezo 5 ya NBC Premier League.

Kocha mkuu wa Simba SC Juma Mgunda ameiongoza Simba kwenye michezo 4 na ameshinda michezo yote

Kocha Juma Mgunda amesema hayo baada ya kikosi chake kuifunga Dodoma Jiji mabao 3-0 jana usiku kwenye mchezo uliochezwa uwanja wa Benjamini Mkapa Dar es salaam.

''Mchezo wa mpira ni mchezo endelevu kila unapopiga hatua unataka kupiga hatua zaidi. Kupata sifa ni rahisi lakini kuilinda sifa ni kazi nyingine. Kwa hiyo sasa hivi tunaenda hatua baada ya hatua siwezi kusema tayari timu ishakuwa lakini kuna hatua ambayo tumetoka kwenda hatua nyingine.’’ Amesema kocha Juma Mgunda.

Mgunda amekiongoza kikosi cha Simba kwenye michezo 4 ya mashindano na ameshinda michezo yote michezo miwili ya ligi kuu na miwili ni ya Ligi ya mabingwa barani Afrika na kuiwezesha timu hiyo kufuzu raundi ya kwanza ya michuano hiyo. Kwenye michezo yote hiyo Simba imefunga mabao 8 na haijaruhusu bao.