Jumamosi , 14th Mei , 2016

Uongozi wa klabu ya soka ya Simba umesema kamwe hautalifumbia macho sakata la mshambuliaji wa timu hiyo Ibrahim Ajib aliyetimkia nchini Afrika Kusini na kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa kinyemela bila ruhusa ya klabu hiyo.

Mshambuliaji wa Simba Ibrahim Ajib [wa mbele] akishangilia moja ya magoli yake akiwa Simba.

Ajibu ambaye ni mshambuliaji chipukizi mwenye kipaji na uwezo wa hali ya juu alikulia katika timu ya pili ya Simba maarufu kama Simba B aliondoka nchini mwishoni mwa juma lililopita ikiwa ni siku moja tangu atolewe kwa kadi nyekundu katika mchezo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania bara dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga mchezo ambao Simba ilikubali kichapo cha bao 1-0 kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na EATV mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya timu hiyo ambaye hakutaka jina lake kuwekwa hadharani amesema kuna taarifa kuwa ndani ya uongozi wa timu hiyo kuna watu wamehusika kwa namna moja au nyingine kufanikisha udhalimu huo kwa maslai yao hivyo wao hawatambui hilo watasimamia kanuni,taratibu na sheria kwa mujibu wa Katiba yao na kamwe hawatalifumbia macho suala hilo kwani kitendo alichokifanya mshambuliaji huyo si cha kinidhamu.

Aidha, kiongozi huyo amesema Ajib ambaye amebakiza msimu mmoja katika mkataba wake wa miaka mitatu na klabu hiyo hawezi kukwepa adhabu japo adhabu yenyewe itategemea na maelezo ya utetezi wake na adhabu inaenda kulingana na kosa husika.

Ajib yuko Afrika Kusini ambako alikwenda akiwa na Meneja wake Juma Ndambile na tayari ameanza vizuri majaribo yake na klabu ya Green Arrows ya nchini humo.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo anasema awali Ajib baada ya kupata ofa hiyo kutoka Sauzi aliuomba uongozi wake umruhusu lakini aligonga mwamba baada ya viongozi wake kumgomea wakimtaka asubiri ligi imalizike ndiyo aende kwenye majaribio hayo ndipo Ajib mwenyewe baada ya kuona hali hiyo itamkosesha fursa ya kucheza soka nje ya nchi hivyo mshambuliaji huyo akaamua kufanya rafu mbaya ya makusudi ili apewe kadi itakayomfaya akose michezo miwili ya ligi hiyo kati ya mitatu na hivyo kutumia mwanya huo kutorokea nchini Afrika Kusini kufanya majaribio.