
Kocha mkuu wa Simba Patrick Aussems (kulia) akiwa na kocha mpya wa viungo Adel Zrane.
Simba imemtambulisha kambini huko Uturuki kocha wa viungo Adel Zrane ambaye ni raia wa Tunisia, akichukua mikoba ya kocha Aymen Hbib ambaye alikuwa sehemu ya benchi la ufundi la kocha Mfaransa Pierre Lechantre.
Adel Zrane ambaye ni pendekezo la Patrick Aussems, amesaini mkataba wa mwaka mmoja kama lilivyo kwa kocha mkuu ambaye naye alisaini mwaka mmoja. Tayari Zrane yupo kambini na amesimamia mazoezi ya viungo leo asubuhi.
Mbali na kocha huyo wa viungo pamoja na Masoud Djuma ambaye ni kocha msaidizi, Simba pia imetangaza watu wengine watakao kuwa kwenye benchi la ufundi ni Kocha wa makipa Mwalami Mohammed na Daktari wa timu Yasin Gembe.
Simba ipo jijini Instabul Uturuki ikifanya maandalizi ya msimu ujao wa ligi kuu pamoja na ligi ya mabingwa Afrika na inatarajiwa kurejea nchini Agosti 5 mpaka 7 tayari kwa tamasha lake la Simba Day ambalo huwa linafanyika Agosti 8 kila mwaka likiwa ni maalum kwa kutambulisha wachezaji wa msimu husika.