Jumatatu , 13th Aug , 2018

Shirikisho la soka Tanzania TFF kupitia kwa bodi yake ya ligi imepangua ratiba ya michezo ya awali ya klabu za Simba na Yanga kutoka katika uwanja wa taifa hadi katika uwanja wa uhuru.

Wachezaji wa Simba na Yanga kwenye moja ya michezo ya timu hizo msimu uliopita.

Akithibitisha taarifa hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB), Boniface Wambura amesema kuwa wamepokea barua kutoka kwa wamiliki wa uwanja wa taifa ambao ni Serikali ikiwataarifu kuwa kuazia Agosti 22 hadi 30 Agosti, uwanja huo utakuwa na matumizi mengine.

Wambura amezitaja mechi ambazo zitahamishwa kutoka katika uwanja wa taifa katika kipindi hicho ni mechi tatu za mwanzo za Simba dhidi ya Prisons, Mbeya City na Lipuli Fc pamoja na mechi ya Mtibwa Sugar dhidi ya Yanga iliyokuwa ichezwe katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Kutokana na mabadiliko hayo, sasa mchezo wa ufunguzi wa ligi wa Simba dhidi ya Prisons, 22 Agosti na Mtibwa Sugar dhidi ya Yanga, 23 Agosti zitachezwa katika uwanja wa Uhuru huku Yanga ikiwa mwenyeji katika mchezo wake.

Pia mchezo wa Simba dhidi ya Mbeya City utakaochezwa, 25 Agosti na ule wa Agosti mosi dhidi ya Lipuli Fc ambao umesogezwa hadi 2,Agosti, michezo yote itachezwa katika uwanja huo wa Uhuru.