Jumapili , 8th Dec , 2019

Mkurugenzi Mtendaji wa Klabu ya Simba Senzo Mazingiza amesema timu hiyo imejipanga kumtangaza Kocha Mkuu wa timu hiyo na benchi lake la Ufundi, ifikapo siku ya Jumatano ya wiki ijayo, ikiwa ni siku chache baada ya timu hiyo kumtimua Kocha Patrick Aussems.

Mkurugenzi Mtendaji wa Klabu ya Simba Senzo Mazingiza

Senzo amesema hayo hayo wakati wa Mkutano Mkuu wa Klabu ya Simba ulofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano ya Kimataifa ya Mwalimu Julius Nyerere, ambapo amesema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri kimataifa.

"Tuna mchezo muhimu na watani wa jadi mwezi Januari. Napenda kuwahakikishia kuwa maandalizi na mambo yote ya mchezo huo yapo tayari. Wachezaji watakuwa kambini na tangazo la nani atakuwa kocha mkuu mpya na benchi la ufundi litatoka rasmi Jumatano ijayo."

Aidha Senzo amesema kuwa "usajili wa wachezaji utafanyika kwa namna tofauti. tutatoa mikataba mirefu kwa wachezaji kwa kuzingatia utaratibu wa kitaalamu, kama unataka kucheza hatua ya nusu fainali ya #CAFCL unahitaji kikosi kitakachoweza kukaa pamoja kwa miaka 3-4."