Jumatatu , 15th Dec , 2014

Klabu ya Simba imekatisha mkataba wa wachezaji wake wawili wa kimataifa, mshambuliaji Amis Tambwe na kiungo Pierre Kwizera baada ya kukamilisha usajili kwa wachezaji watatu wa kimataifa Daniel Sserunkuman, Simon Sserunkuma na Beki Juuko Murushid.

Akizungumza na East Africa Radio, Afisa Habari wa Klabu hiyo, Humphrey Nyasio amesema usajili huo unatarajiwa kufungwa leo na usajili umetokana na mapendekezo ya kocha hivyo bado wanaangalia hitaji la kocha kabla ya saa 6 usiku muda wa kufungwa dirisha hilo la usajili.

Nyasio amesema, Suala la kumsajili mchezaji wa klabu ya Yanga Hamis Kiiza hajasikia kama mchezaji huyo alishafanya mazungumzo na kamati ya Usajili ya Simba lakini usajili wa mchezaji yoyote inategemea na kocha anahitaji mchezaji gani kutokana na nafasi.

Nyasio amesema Timu hiyo inatarajia kuanza mazoezi ya kawaida Jumatano ya wiki hii ikijiandaa na Ligi kuu Tanzania lakini timu hiyo itaingia kambini Rasmi ikiwa ni sehemu ya kufanya maandalizi mazuri ya Ligi hiyo yenye ushindani mkubwa.