Alhamisi , 2nd Sep , 2021

Sports Countdown ya East Africa Radio leo Septemba 3, 2021. Moja ya Stori kubwa leo ni Cristiano Ronaldo aweka rekodi mpya ya ufungaji kwa timu za taifa, na Taifa stars kuumana na Congo mchezo wa kuwania kufuzu kombe la Dunia.

Cristiano Ronaldo amefunga mabao 111 kwenye michezo 180 akiwa na kikosi cha timu ya taifa ya Ureno

6. Ni idadi ya wachezaji waliosajiliwa na washika bunduki wa jiji la London klabu ya Arsenal kwenye dirisha la usajili la majira ya joto lililofungwa Agosti 31, 2021, na idadi hiyo ya wachezaji imeifanya klabu hiyo kuwa ndio timu iliyotumia pesa nyingi kusajili wachezaji kwenye orodha ya timu za EPL zilizotumia fedha nyingi kusajili wacheza jumla ya pesa ilitumia Arsenal ni pauni milioni 156.8, ambayo imetumika kusajili wachezaji 6, ambao ni Nuno Tavares, Ben White, Martin Odergaard, Albert Sambi Lokonga, Aaron Ramsadale, na Takihiro Tomiyasu.

Timu nyingine zilizotumia pesa nyingi kwenye EPL ni Mancheater United inashika nafasi ya pili ikiwa imetumia pauni milioni 133.7, Manchester City imetumia pauni milion 100 na Chelsea imetumia pauni milion 97.

Licha ya kuwa vinara kwenye ordha ya timu zilizotumia pesa nyingi kununua wachezaji lakini Arsenal inayoburuza mkia kwenye msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kufungwa michezo yote mitatu ya mwanzo wa Ligi.

 

5. Ni sawa na idadi ya michezo ambayo kocha wa Timu ya taifa ya Tanzania taifa Stars Kim Poulsen raia wa Denmark atakuwa amekiongoza kikosi cha hicho kwenye michezo ya mashindano na ya kirafiki tangu atangazwe kuwa kocha wa kikosi hicho akichukua nafasi ya Etienne Ndayiragije mnamo Februari 15 mwaka huu.

Na hii leo Jioni majira ya saa 10 Kocha Kim atakuwa akiiongoza Taifa stars kwenye mchezo wake wa tano dhidi ya timu ya taifa ya Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo ukiwa ni mchezo wa Kundi J wa kuwania kufuzu fainali za kombe la Dunia zitakazo fanyika nchini Qatar mwaka 2022. Katika michezo 4 ya awali kocha Kim Poulsen ameshinda michezo miwili Dhidi ya Malawi na Libya lakini pia amefungwa michezo miwili dhidi ya Kenya na Equatorial Guinea.

 

4. Ni idadi ya mataji ya Grandslams aliyoshinda Mwanadada Naomi Osaka ambaye pia ni bingwa mtetezi wa michuano ya wazi ya tennis ya Marekani US Open, na Mwanadada huyo raia wa Japan ataanza safari yake ya kutetea ubingwa wa michuano hiyo dhidi ya Leylah Fernandez kwenye roundi ya tatu baada ya mpinzani wake Olga Danilovic kujitoa kutokana na sababu za kimatibabu katika roundi ya pili hivyo kumfanya Naomi kufuzu roundi ya tatu bila kucheza yani walkover.

Osaka ni Bingwa mara mbili wa michuano ya US Open na Australian Open, atacheza dhidi ya Leylah ambaye amefuzu roundi ya tatu baada ya ushindi wa set 2 mfululizo 7-5 7-5 dhidi ya Kaia Kanepi kwenye mchezo wa raundi ya pili. Na mchezo wa Osaka na Leylah utachezwa kesho September 3, 2021.

3. Ni idadi ya siku zilizobaki kabla ya michuano ya Olimpiki kwa watu wenye ulemavu Paralympic kumalizika Septemba 5 huko Tokyo Japan. Na mpaka sasa taifa la China ndio linaloongoza kwa kushinda medali nyingi likiwa na medali 152, huku 71 zikiwa za dhahabu, na Uingereza imeshinda Medali 90, 32 za dhahabu ikiwa ya pili kwa kushinda medali nyingi, na timu ya Olympic ya Urusi imeshinda medali 89, 32 ni dhahabu.

Michezo hii ya Paralympic ilianza Agust 24 na imejumuisha jumla ya wanamichezo 4537 kutoka mataifa 163. Na mtanzania Ignance Madumla Mtweve alishatupa karata yake kwenye mchezo wa kurusha kisahani na alimaliza nafasi ya 8.

 

2. Ni miaka aliyofanya kazi Antonio Nugaz ndani ya klabu ya Yanga kama afisa muhamasishaji na msemaji wa kikosi hicho cha mabingwa wa Kihistoria wa Tanzania bara, na hapo jana uongozi wa Yanga ulitangaza rasmi kuachana na Nugaz baada ya mkataba wake wa miaka miwili kuisha na klabu hiyo umeweka wazi kuwa haitamuongezea mkataba.

Kwa upande wake Nugaz ameushukuru uongozi wa Yanga kwa kipindi choto alichofanya kazi na amewatakia kila la kheri kwenye majukumu ya kuisogeza mbele katika mafanikio klabu hiyo.

Lakini pia Yanga kupitia Kamati yake ya utendaji chini ya Mwenyekiti Dr Mshindo Msola, imewateua wajumbe 8 wanaounda kamati ya Mashindano ambayo Mwenyekiti wake ni Rodgers Gumbo, na baadhi ya wajumbe hao ni Davis Mosha, Seif Magari, Abdallah Bin Kleb, Arafat Haji, Eng Hersi Said, Pelegrinius rutayunga, Hamed Islam na Lucas Mashauri.

 

1. Ni nafasi anayoshikilia Cristiano Ronaldo kwenye orodha ya wachezaji waliofunga mabao mengi kwenye timu za Taifa Duniani akiwa na mabao 111. Ronaldo ambaye ni mchezaji bora wa Dunia mara 5 amefekia rekodi hiyo baada ya kufunga mabao mawili jana usiku kwenye mchezo wa kuwania kufuzu kombe la Dunia ambapo timu ya taifa ya Ureno ilifanikiwa kuinyika timu ya Jamuhuri ya Ireland kwa mabao 2 - 1 kwenye mchezo wa Kundi A na Cristiano Ronaldo ndio alikuwa mfungaji wa mabao yote ya Ureno kunako dakika ya 89 na ya 106 na sasa anakuwa amefunga mabao 111 yakiwa ni mengi kuliko mchezaji yoyote yule kwenye ngazi ya timu ya taifa na kaweka rekodi hiyo ya mabao katika michezo 180 akiwa na kikosi cha Ureno.

Mabao hayo mawili ya Ronaldo mwenye umri wa miaka 36 yamemfanya aivuke na kuivunja rekodi ya mabao 109 ambayo alikuwa mefunga Ali Daei mchezaiji wa zamani wa timu ya taifa ya Irani. Na Kabla ya mchezo huo Ronaldo alikuwa na mabao 109 sawa na Ali lakini kwa sasa yeye ndio kinara.