Alhamisi , 22nd Jul , 2021

Stori sita (6) za michezo (Sports Countdown) leo asubuhi Julai 22, 2021. kwenye Supa Breakfast ya East Africa Radio kuanzia Saa 1:15 Asubuhi, ambapo kila stori inatokana na namba 1 mpaka 6. Na moja ya stori kubwa leo ni David alaba apewa jezi namba 4, Tanzania yaifunga Congo.

Wachezaji wa Tanzania wanaounda kikosi cha timu ya taifa

6. Ni idadi ya tuzo za mchezaji bora wa Dunia kwa wanawake alizoshinda Marta Vieira da Silva wa Brazili, ambaye jana aliweka rekodi kwenye michezo ya Olympic upande wa mpira wa miguu kwa kuwa mchezaji wa kwanza upande wa wanaume na wanawake kufunga magoli kwenye michuano mitano mfululizo ya Olimpiki.

Marta mwenye umri wa miaka 35 ameweka rekodi hiyo baada ya kufunga mabao mawili kwenye mchezo wa kundi F dhidi ya timu ya taifa ya China kwenye ushindi wa mabao 5- 0 waliopata Brazil. Marta anatajwa kuwa ni mchezaji bora wa kike kuwahi kutokea na mchezo wa jana ulikuwa wa 160 akiwa na kikosi cha timu ya taifa ya Brazil na mabao hayo mawili yamemfanya afikishe mabao 111, na bado ananafasi ya kuweka rekodi nyingine kwenye michezo miwili ya makundi inayofata dhidi ya Uholanzi na Zambia.

5. Ni idadi ya mabao yaliyofungwa kwenye mchezo wa mtoano (play off) kati ya Transt Camp dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Dimba la Uhuru Dar es salaam, ambapo mshambuliaji wa Mtibwa Sugar Ibrahim Ahmada Hilika alifunga mabao matatu yani Hat trick kwenye mchezo huo wa mtoano wa kuwania nafasi ya kucheza Ligi Kuu msimu ujao wa 2021-22, katika mchezo huo Mtibwa iliibuka na ushindi wa mabao 4-1, ukiwa ni mchezo wa mkondo wa kwanza ambao Transt ndio walikuwa wenyeji bao jingine la Mtibwa limefungwa na Kelvin Sabato wakati lile la Transt Camp limefungwa na Wazanga.

Mchezo mwingine wa Play off ulichezwa kule jijini Mwanza ambapo Coastal Union ya Tanga walikuwa ugenini kucheza dhidi ya Pamba ya Mwanza na mchezo huo ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2. Na michezo ya marejeano itachezwa Julai 24, 2021. Ambapo Mtibwa watakuwa wenyeji wa Transt Camp na Coastal watakuwa katika dimba la Mkwakwani Tanga kuwakaribisha Pamba.

4. Ni namba ya Jersey atakayovaa beki mpya wa Real Madrid David Alaba, ambaye ametambulishwa rasmi katika klabu hiyo na kukabidhiwa Jersey namba 4 ambayo awali ilikuwa ikivaliwa na nahodha wa zamani wa klabu hiyo Sergio Ramos ambaye amejiunga na PSG ya Ufaransa baada ya kumaliza mkataba mwishoni mwa msimu uliopita, Ramos aliitumikia Madridi kwa miaka 16.

Alaba amejiunga na Real Madrid akitokea Bayern Munich na amesaini mkataba wa miaka mitano, ni mchezaji mzoefu na mshindi ambaye moja kwa moja anatazamwa kama mbadala wa Sergio Ramos kuja kuwa kiongozi wa safu ya ulinzi akiambatana na Raphael Varane. David Alaba raia wa Austria ana umri wa miaka 29, kwa ujumla ameshinda mataji 27 akiwa na kikosi cha Bayern Munich ukiwemo ubingwa wa Ligi Kuu Ujerumani Bundesliga mara 10 na ule wa klabu bingwa ulaya mara 2.

3. Ni orodha ya waamuzi wa ndani watakao chezesha mchezo wa fainal ya kombe la Azam Sports Federation Cup kati ya Simba na Yanga mchezo utakao chezwa Julai 25, 2021, katika Dimba la Lake Tanganyika mkoani Kigoma.

Na majina ya waamuzi hao tayari yamewekwa hadharani na shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF. Na mwamuzi wa kati ni Ahmed Arajiga kutoka Manyara, mwambuzi msaidizi namba moja yani Line 1 ni Ferdnand Chacha kutoka Mwanza, msainizi namba mbili Line 2 ni Mohamed Mkono wa Tanga na mwamuzi wa akiba yani fourth official ni Elly Sassi wa Dar es salaam.

Mchezo huu utachezwa kuanzia majira ya Saa 10 kamaili jioni. Na tayari kikosi cha Yanga kimeshaondoka Jiji Dar es salaam kuelekea Kigoma Leo Asubuhi.

2. Ni miaka aliyosaini kiungo wa kimataifa wa Kenya Kenneth Muguna wa kuitumikia klabu ya Azam FC, mkataba utakao malizika mwaka 2023, anajiunga na Azam akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na klabu ya Gor Mahia ya Kenya.

Kenneth amesema amefurahi kujiunga na Azam FC, na anaamini kuwa klabu hiyo ni kubwa nchini Tanzania na yupo tayari kuanza kazi, huu ni usajili wa nne kikosi hicho cha waoka mikate wanautangaza baada ya kukamilisha usajili wa Edward Manyama, Rodgers Kola na Charlse Zulu.

1. Ni bao pekee lilofungwa na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania chini ya umri wa miaka 23 Reliant Lusajo dakika ya 66 kwenye mchezo wa hatua ya makundi dhidi ya timu ya taifa ya Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo mchezo ambao Tanzania imeibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye michuano ya wachezaji chini ya umri huo ukanda wa Afrika mashariki na kati yani CECAFA senior Challenge U 23, michuano hiyo inayoendelea nchini Ethiopia.

Baada ya ushindi huo sasa Tanzania ndio vinara wa kundi A wakiwa na Alama 3, wakifuatiwa na Uganda wenye alama 1 na kongo ndio wanao buruza mkia wakiwa na alama 1 katika michezo miwili. Mchezo unaofata Tanzania itashuka dimbani dhidi ya Uganda Julai 24, 2021.