Jumanne , 20th Jul , 2021

Stori sita (6) za michezo (Sports Countdown) leo asubuhi kwenye Supa Breakfast ya East Africa Radio kuanzia Saa 1:15 Asubuhi, ambapo kila stori inatokana na namba 1 mpaka 6. Na moja ya stori kubwa leo ni viingilio vya mcheo wa Yanga na Simba vyatangazwa, Chelsea kumsajili Halaand.

Wachezaji wa Simba na Yanga wakiwania mpira kwenye moja ya michezo msimu huu wa 2020-21

6. Ni idadi ya mataji ya ligi kuu iliyoshinda klabu ya Chelsea ya England na katika harakati za kuhakikisha inashinda taji la saba kuelekea msimu ujao wa 2021-22 matajiri hao wa jiji la London watapeleka ofa yao ya mwisho yakutaka kumsajili Mshambuliaji wa Borussia Dortmund Erling Braut Håland wiki hii.

Inaripotiwa kuwa Chelsea watamjumuisha mshambuliaji wao Timo Werner ambae alifunga mabao 6 tu ya Ligi na 12 kwenye michuano yote kwenye ofa yao ya pili na kiasi cha pesa ikiwa sehemu ya kuwashawishi Dortmund ambao wanaonekana hawapo tayari kumuuza mshambuliaji huyo.

Awali iliripotiwa kuwa mabingwa hao wa ulaya Chelsea waliwajumuisha winga Callum Hudson-Odoi na mshambuliaji Tammy Abraham kama sehemu ya ofa lakini Borussia waliikataa ofa hiyo ikidaiwa kuwa hawapo tayari kuwapoteza wachezaji wao bora wawili ndani ya msimu mmoja baada ya kumuuza Jadon Sancho kwenda ManchesterUnited.

Halaand mwenye Umri wa miaka 20 thamani yake sokoni inatajwa kuwa ni pauni milioni 170 zaidi ya bilioni 538 kwa pesa za kitanzania, na msimu uliopita alifunga mabao 41 kwenye michezo 41.

5. Ni idadi ya mabao aliyofunga mshambuliaji soufiane Rahimi wa Raja Casablanca kwenye michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika msimu wa 2020-21 ambapo alikuwa sehemu ya mafaniko ya kikosi hicho kutwaa ubingwa wa michuano hiyo, kufuatia kiwango bora alichoonyesha msimu huu kocha wa Al Ahly Pitso Mosimane amethibitishwa kuwa klabu hiyo inamfuatilia mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25 raia wa Morocco ili waweze kumsajili kuelekea msimu ujao wa 2021-22, na kwa mujibu wa taarifa Al Ahly wapo tayari kulipa dola milion 2 ambayo ni zaidi ya bilion 4 kwa pesa za kitanzania kama ada ya uhamisho ya mchezaji huyo lakini klabu yake ya Raja Casablanca inaripotiwa ipo tayari kumuuza kwa dola milion 3 ambayo ni zaidi ya bilion 6.

4. Ni idadi ya michezo ambayo Simba na Yanga watakuta msimu huu kwenye michuano yote ambapo mchezo wa nne msimu huu timu hizi zitacheza Julai 25 huko Kigoma katika dimba la Lake Tanganyika ukiwa ni mchezo wa Fainali ya michuano ya Azam Sports Federation Cup, na kuelekea mchezo huo shirikisho la soka nchini TFF limetangaza viingilio vya mchezo huo ambavyo ni elfu thelathini (30,000) elfu ishirini (20,000) elfu kumi na tano (15,000) na elfu kumi (10,000) na jumala ya mashabiki watakao hudhuria mchezo huo ni mashabiki elfu kumi na nane (18,000).

Michezo mingine mitatu iliyopita timu hizi kukutana msimu huu ni miwili ya ligi kuu Tanzania bara ambapo Yanga ilishinda mchezo mmoja kwa bao 1-0, na mchezo mwingi ulimalizika kwa sare ya bao 1-1, na mchezo mwingine ni fainali ya mapinduzi CUP ambapo Yanga walishinda kwa mikwaju ya penati (4-3).

3. Ni idadi ya wanamichezo waliokutwa na maambukizi ya Virusi vya Corona kwenye kijiji cha wanamichezo watakao shiriki katika michezo ya Olympic huko Tokyo Japan itakayoanza Julai 23 mwaka huu,

Idadi hiyo imefikia baada ya mchezaji wa mpira wa wavu wa ufukweni yani beach Volleyball Ondřej Perušič wa Jamuhuri ya Czech kukutwa na maambukizi ya virusi hivyo ingawa inaripotiwa alipata chanjo ya Corona. Siku ya Jumapili iliripitiwa kuwa wachezaji wawili wa timu ya mpira wa miguu ya Afrika kusini walikutwa na maambukizi hayo licha yakupata chanjo kabla ya kuelekea Japan.

Olympic 2020, itahusisha jumla ya mataifa 206 na jumla ya wanamichezo 11238 wanatarajiwa kushiriki katika michezo 33 tofauti.

2. Ni sawa na idadi ya miaka aliyosaini mshambuliaji Rodgers Kola katika mkataba wa kujiunga na klabu ya Azam FC ya Dar es salaam ambapo mkataba huo utamalizika mwaka 2023, Kola anajiunga na Azam FC akiwa mchezaji huru baada ya kuachana na klabu ya Zanaco, msimu uliopita alifunga jumla ya mabao 14 kwenye michuano yote.

Huu ni usajili wa tatu Azam wanakamilisha baada ya kukamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji Charlse Zulu raia wa Zambia ambaye naye alisaini mkataba wa miaka miwili akitokea Cope Town City ya Afrika Kusini, mchezaji mwingine ni Edward Manyama ambaye alijiunga kwa mkataba wa miaka 3 akitokea Ruvu shooting.

1. Ni nafasi anayoshikilia Lewis Hamilton kwenye orodha ya waendesha magari ya Langa langa (F1) waliochukua ubingwa mara nyingi sambamba na Michael Schumacher wote wakiwa wametwaa ubingwa wa Dunia mara 7, licha ya rekodi hiyo na mafanikio hayo Hamilton amejikuta akikumbana na ubaguzi wa rangi kutoka kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii Facebook, tweeter na Instagram.

Hamilton anakumbana na kadhia hiyo baada ya kutuhumiwa kumchezea madhambi dereva wa Red Bull Max Verstappen na kusababisha ajali ambayo ilipelekea Max kushindwa kuendelea na mbio hizo na kukimbizwa Hospital, tukio hilo limetokea kwenye mbio za Great Britain GP kwenye njia ya Silverstone siku ya Jumapili.

Baada ya matukio hayo wamiliki wa Facebook na Instagram wamesema wameanza kuchukua hatua kupambana na watu wote wanaofanya vitendo hivyo ikiwemo kuzifunga account lakini pia wameshafuta zaidi ya Comment 1000 ambazo zilikuwa zikionyesha ubaguzi dhidi ya Hamilton.