Jumatano , 28th Jun , 2017

Joto la mashindano ya mpira wa kikapu ya Sprite BBall Kings hatua ya Robo fainali limezidi kupanda kwa timu shiriki nane zinazowania kitita cha shilingi milioni 15 zilizowekwa mezani, zikijiandaa kwa mitanange hiyo.

Mchezaji wa Kurasini Heat Yassin Chona ambaye ndiye kinara kwa ufungaji wa alama 64 katika mashindano hayo, amesema licha ya kuwania tuzo ya mchezaji bora, lakini lengo lake amelielekeza katika kuisaidia timu yake kuifunga Kigamboni Heroes ili watinge nusu fainali hapo jumamosi.

Katika hatua nyingine Chona amewataka mashabiki wa timu yake kujitokeza kwa wingi siku ya Jumamosi ya Julai mosi mwaka huu katika viwanja vya chuo kiku cha Dar es salaam ili kushuhudia namna timu yao itakavyokua ikionesha mchezo mzuri dhidi ya Kigamboni Heroes.

Mechi za robo fainali za Sprite BBall Kings zitarajiwa kupigwa kuanzia majira ya saa mbili asubuhi ambapo timu za The Fighter itakipiga na Mchenga B Ball Stars, Flying Dribblers itaumana na Oysterbay, Dream Chaser dhidi ya TMT nayo Kurasini Heat itapepetana na Kigamboni Heroes.