
Nembo ya Mtibwa Sugar na Northern Dynamo
Northern Dynamo ni mabingwa wa Airtel Cup msimu wa 2017-2018, pia katika ligi ya Shelisheli, Nothern Dynamo imecheza michezo 18 mpaka sasa, ikiwa imeshinda mechi nne, imefungwa mechi 11 na kutoka suluhu michezo mitatu ambapo inashika nafasi ya 9 katika msimamo wa ligi hiyo yenye timu 12, ikiwa na alama 15.
Kwa upande wa mwenyeji Mtibwa Sugar, yenyewe imecheza mechi 14 mpaka sasa katika ligi kuu Tanzania bara TPL, ikiwa imeshinda michezo saba, imefungwa michezo mitano na kutoka sare mechi mbili, huku ikiwa katika nafasi ya nne katika msimamo.
Kutokana ubora huo katika ligi zao, Mtibwa Sugar inaonekana kuwa bora zaidi ya Northern Dynamo, jambo ambalo linawapa nafasi kubwa zaidi ya kuibuka na ushindi katika mchezo wa leo ikizingatiwa kuwa iko katika ardhi ya nyumbani.
Timu hizi hazijawahi kukutana katika michuano ya kimataifa, na hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Mtibwa Sugar kucheza michuano hiyo tangu mwaka 2003, ilipofungiwa na Shirikisho la Soka barani Afrika CAF kushiriki michuano hiyo baada ya kushindwa kusafirisha timu.
Viingilio vilivyotangazwa kwaajili ya kushuhudia mtanange huo ni, Sh 2,000 kwa viti vya kawaida pamoja na Sh 3,000 kwa viti vya mzunguko.
Endapo itafanikiwa kuibuka na ushindi katika mechi zote mbili, mechi ya nyumbani na ya ugenini, Mtibwa Sugar itasonga mbele katika hatua ya pili kabla ya kuingia katika hatua ya makundi ya michuano hiyo. Kila la heri wakata miwa wa Morogoro wawakilishi wa Tanzania katika kombe la shirikisho barani Afrika.